Kahawa Veterani yatinga kwa mbinde nusu fainali Nyerere Day Morogoro

KAHAWA Veterani Fc ya Visiwani Zanzibar imefuzu kwa mbinde kwa kutinga hatua ya nusu fainali michuano ya Nyerere Day 2022 Morogoro mbele ya Gwasa ya Dar es Salaam baada ya kuichapa jumla ya bao 12-11 kwa njia ya matuta katika mchezo mkali wa robo fainali uwanja wa Shujaa Morogoro.

Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuamuliwa kumpata mshindi kwa njia ya matuta na Gwasa Fc ikitumbukiza kambani mipira 10 na wapinzani wao wakitikisa nyavu 11 na kufanya mchezo huo umalizike kwa idadi kubwa ya mabao 12-11 na Kahawa kusonga hatua ya nusu fainali.

Akizungumza na Mwanaspoti katika michezo hiyo inayoendelea mjini hapa, Msemaji wa Nyerere Day Morogoro 2022, Shaibu Mohamed amesema michuano hiyo imekuwa na msisimuko kutokana na timu nyingi kujiandaa na kutengeneza upinzani mkali.


Shaibu amesema timu 18 zinashiriki zikiwana wachezaji waliotamba enzi zao ligi za ushindini ngazi ya vilabu na timu ya taifa akiwemo Haruna Moshi Bobani, Faustine Lukoo, Abdallah Juma, Victor Costa, John Kanakamfumo, Mokili Rambo, Fred Hagai na wengine wengi.

“Baada ya kumalizika kwa michezo ya makundi robo fainali Kahawa Veterani ilimenyana na Gwasa Veterani na mchezo huo kumalizika kwa jumla ya bao 12-11 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 na Kahawa kutinga nusu fainali na itakutana na Mfinga Veterani.”amesema Shaibu.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Morogoro Veterani ilitolewa nishai kwa kuaga kwa kukumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mafinga Veterani kwa bao la Mussa Mwakisu aliyezima ndoto za wenyeji hao kutetea ubingwa huo dakika ya 28 na kujikuta wakiinamisha vichwa chini kwa kipigo hicho.

Robo fainali nyingine Kabuka Veterani Fc ya Tanga ilikufa kiume dhidi ya Watumishi Veterani Dodoma kwa kuondolewa kwa bao jumla ya bao 3-2 kwa penalti baada ya suluhu ya 0-0 huku Suka Veterani ya Dar es Salaam ilisonga hatua ya nusu fainali kwa kuichapa Eimu Zanzibar bao 1-0.

Kiungo wa zamani wa Simba Sc na Yanga Sc, Haruna Moshi Boban alikuwa sihala ya ushindi kwa Suka Veterani kutokana na uzoefu wake dhidi ya wapinzani wao katika kugawa mipira iliyoleta hekaheka langoni mwa wapinzani wao.