Kahata aanika siri zake na Gomes

Saturday June 05 2021
KAHATA PIC
By Thobias Sebastian

KIUNGO fundi wa mpira wa Simba, Francis Kahata amewaaga mashabiki wa klabu hiyo, lakini akifichua siri yake na Kocha Didier Gomes.

Kahata ameachana rasmi na Simba baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Akizungumza na Mwanaspoti jana kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, Mkenya huyo alisema tayari amekutana na Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez na kumalizana naye baada ya kumwambia hawatamuongezea mkataba mpya.

“Awali nilishajiandaa na jambo hilo na hata baada ya kuniambia wazi wazi wala sikushtuka, ingawa ni moja ya taarifa mbaya na changamoto ya kisoka ambayo nimewahi kupitia katika maisha ya soka,” alisema Kahata na kuongezea;

“CEO aliniambia watanipa stahiki zangu zote ambazo nilitakiwa kupata ndani ya mkataba wangu hadi utakapomalizika Julai 30 ikiwamo posho nyinginezo na kimsingi nilitamani kubaki hapa, ila sina jinsi licha ya miezi yangu sita ya mwisho Simba imekuwa migumu mno.”

Kahata pia alifichua licha ya kukutana na hali ya sintofahamu kwenye miezi sita ya mwisho ya mkataba wake, lakini alisema amefurahi kufanya kazi na Kocha Didier Gomes, aliyekuwa akimtia moyo na kumfanya ajitume uwanjani licha ya changamoto alizopitia klabuni.

Advertisement

Alisema Gomes alipofika nchini kufundisha Simba, alipata muda wa kuzungumza naye na kumueleza kufurahi kufanya naye kazi, kwani anamjua tangu akiwa Gor Mahia.

“Hata hivyo, baada ya muda alifahamu situmiki katika mashindano ya ndani lilikuwa ni suala lililomshangaza na alipokuja kuniuliza nilimjibu hata mie nashangaa, ila alinitia moyo na kuniandaa kisaikolojia kiasi cha kutojisikia vibaya,” alisema Kahata na kuongeza;

“Gomes alikuwa akitumia muda wake kwenye maandalizi ya mechi hasa zile za kimataifa, kunitengeneza kiakili na kunitia moyo, pia alikuwa akinipa nafasi kikosini na juzi wakati timu inaenda Mwanza kwa mchezo wa Ruvu Shooting (uliopigwa jana) nilizungumza naye.”

Kahata alisema, Gomes alimwambia baada ya kutoka Mwanza kucheza na Ruvu atakaporudi Dar es Salaam angefanya kikao na viongozi ili kujua hatma yangu kwa msimu ujao, lakini kabla ya muda huo kufika ndio akaitwa na uongozi kunipa taarifa za kuachana nao rasmi.

“Sijapata muda wa kuongea naye na pengine hajui kama sitakuwa tena Simba, ila kabla ya kuondoka Tanzania, nitakaa naye na kumueleza kila kitu, kisha nitaenda nyumbani kukaa kwanza na familia yangu na kupumzika,” alisema Kahata aliyesajiliwa Simba Julai, 2019 na kuifungia mabao manne katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Advertisement