Kagoma ampa tuzo Chasambi
Muktasari:
- Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuhojiana na Kagoma alifurahia kupata tuzo hiyo, ambayo alisema anaidediketi kwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo,Ladack Chasambi.
KIUNGO mkabaji wa Simba,Yusuf Kagoma amefichua jambo lililojicha nyuma ya tuzo ya mchezaji bora wa mechi aliyopata baada ya timu hiyo kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuhojiana na Kagoma alifurahia kupata tuzo hiyo, ambayo alisema anaidediketi kwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo,Ladack Chasambi.
Kagoma alisema lilikuwa ombi la Chasambi la siku nyingi, kuona anapata tuzo hiyo na baada ya kupata anaamini kiu ya rafiki yake imetibika.
"Tuzo hii naidediketi kwa rafiki yangu Chasambi kila nikicheza mechi ananiambia anatamani kuniona nachukua mchezaji bora wa mechi, nilipoipata basi nimwambie ni spesho kwake aliyekuwa anatamani kuona hilo," alisema Kagoma na kuongeza;
"Pia nimefarijika kuona wengine wanatambua ninachokifanya uwanjani."
Ukiachana na hilo alisema mechi dhidi ya Mtibwa Sugar waliyoifunga mabao 3-0 ilikuwa ngumu, lakini jambo la msingi ni kupata pointi tatu.
"Kidogo uwanja ulikuwa changamoto, ukipiga mipira ilikuwa haitembei, ila la msingi zaidi ni sisi kuvuna alama tatu, baada ya mzunguko wa kwanza kugawana pointi moja moja," alisema.
Mkuu wa kitengo cha Habari na mawasiliano Simba, Ahmed Ally alizungumzia tuzo ya Kagoma:" Siyo rahisi kuona nafasi kama ya Kagoma mchezaji anachukua tuzo, hilo ni jambo jema kuona wameboresha hilo."