Kagere bado yupo sana Ligi Kuu, atua Singida

Thursday August 04 2022
kagere pic
By Damian Masyenene

KWA waliodhani Meddie Kagere hatoonekana tena baada ya kuachwa na Simba watakuwa wamejidanganya sana, kwani mchezaji huyo ataonekana sana Ligi Kuu baada ya kusajiliwa na Singida Big Stars iliyopanda daraja.

Singida Big Stars imemtambulisha nyota huyo leo Agosti 4 saa 9 mchana mbele ya mashabiki wake katika tamasha la Singida Big Day linaloendelea kwenye uwanja wa Liti mkoani Singida.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ametambulishwa wa mwisho katika orodha ndefu ya wachezaji wa kikosi cha Singida Big Stars kilichotambulishwa leo huku akipigiwa shangwe kubwa na mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo.

Mshereheshaji wa tamasha hilo, Antonio Nugaz wakati akitambulisha wachezaji alimuita mchezaji wa mwisho kwenye orodha, Said Ndemla huku mashabiki wakijua orodha imekamilika ghafla akamuita Kagere ambaye alitoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwa amevaa jezi za timu hiyo na kuelekea uwanjani akiwapungia mkono mashabiki.

Kagere ni miongoni mwa wachezaji watatu walioondolewa kikosini dakika za mwisho na kocha wa Simba, Zoran Maki baada ya kutoridhishwa na kiwango chao, wengine ni Chris Mugalu na Thadeo Lwanga ambapo anaungana na nyota wengine waliowahi kukipiga pamoja Simba, Paschal Wawa, Said Ndemla na Nicolas Gyan.

Singida Big Stars inafanya tamasha hilo kutambulisha kikosi chake cha msimu ujao, jezi, benchi la ufundi huku likinogeshwa na burudani ya muziki kutoka kwa msanii, Harmonize na Ibraah.

Advertisement

Ambapo tamasha hilo litahitimishwa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanaco FC ya nchini Zambia utakaoanza saa 10 jioni.

Advertisement