Kagere afunguka laivu

BAADA ya kuwepo kwa maneno mengi juu ya straika wa Simba, Meddie Kagere kutokucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs mwenyewe amefunguka.

Kagere ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Ambalo lipo katika akili yangu ni kuhakikisha kila nikipewa nafasi ya kucheza nafanya vizuri kwa kutoa mchango kwa timu kupata kile ambacho tunahitaji.”

“Ndio maana ikitokea hata nimekaa nje bila kucheza huoni naonyesha tofauti yoyote ila ikitokea nimepewa nafasi ya kucheza tu huwa napenda kufanya mambo kama ambavyo yaliyotokea katika mechi ya Dodoma Jiji.

“Binafsi si mtu ambaye napenda kuongea zaidi bali natamani kufanya vitendo kama ambavyo kazi yangu inahitaji huwa nashukuru Mungu kila nikipata nafasi ya kucheza huwa hivyo,”alisema Kagere na kusisitiza hana tofauti zozote na Kocha na anaheshimu uamuzi wowote wa benchi la ufundi.

Katika hatua nyingine Kagere alisema amepanga kufunga mabao mengi zaidi katika kombe hilo la FA pamoja na Ligi Kuu Bara ambalo alikuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo.

Kagere alisema kwenye kombe la FA amefunga mabao matatu akitokea amepewa nafasi ya kucheza anatamani kuongeza idadi hiyo ili kuwa mengi zaidi.

“Jukumu langu ni kufunga mabao mengi zaidi ya haya niliyokuwa nayo katika mashindano yote ili kuisaidia timu yangu kufanya vizuri na kufikia malengo ambayo tumejipangia,” alisema Kagere.

Kagere ndio mfungaji bora wa ligi mara mbili mfululizo na msimu huu anashika nafasi ya pili akiwa na mabao 11, huku kinara akiwa mshambuliaji wa Azam, Prince Dube mwenye mabao 14.