Kagera, Mbeya City kazi ipo

Kagera, Mbeya City kazi ipo

Muktasari:

  • LIGI Kuu Bara inarejea tena upya baada ya kusimama kwa zaidi ya mwezi mmoja kupisha mechi za kimataifa za timu za taifa na siku 21 za maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, huku kibarua kizito kikiwa kwa Kocha Mkuu mpya wa Kagera Sugar, Francis Baraza anayevaana na Mbeya City ikiwa ni mechi yake ya kwanza na timu hiyo.

LIGI Kuu Bara inarejea tena upya baada ya kusimama kwa zaidi ya mwezi mmoja kupisha mechi za kimataifa za timu za taifa na siku 21 za maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, huku kibarua kizito kikiwa kwa Kocha Mkuu mpya wa Kagera Sugar, Francis Baraza anayevaana na Mbeya City ikiwa ni mechi yake ya kwanza na timu hiyo.


Kocha Baraza ataanza kibarua chake cha kwanza leo katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City ambayo watakuwa ugenini katika uwanja wa Sokoine Mbeya.


Baraza anasema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa upande wake kutokana anakwenda kucheza na timu ambayo haipo katika wakati mzuri kwenye msimamo wa ligi lakini watakuwa ugenini.


"Ukiangalia hata nasi hatupo mahala salama ila tumejindaa ili kupata ushindi na kujiondoa katika mazingira ambayo tupo," amesema.


"Kikubwa mechi itakuwa yenye ushindani na timu ambayo itafanya vizuri katika eneo la kiungo hiyo hiyo ndio itafanikiwa kupata pointi tatu," anasema Baraza ambaye alichukuwa na Kagera akitokea Biashara United.


Baada kusimama takribani mwezi mmoja Ligi Kuu Bara itarejea kesho (Alhamisi) kwa kuchezwa mechi mbili kati ya Mbeya City ambao watakuwa nyumbani dhidi ya Kagera Sugar na mchezo huo utaanza saa 8:00 mchana.


Mechi hiyo baada ya kumalizika saa 10:00 jioni kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Namungo ambao watakuwa katika Uwanja wa Majaliwa na watawakalibisha walima mpunga wa Mbeya, Ihefu Fc.


Mbeya City wanaingia katika mechi hiyo wakiwa katika nafasi ya 16, timu tatu kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi wakiwa wamecheza mechi 23, wameshinda tatu, wametoka sare 11, wamefungwa tisa, wamefunga mabao 15, wamefungwa mabao 25, wamekusanya pointi 20.


Wakati wapinzani wao Kagera Sugar wapo nafasi 13, wamecheza mechi 24, wameshinda sita, wametoka sare saba, wamefungwa 11, wamefunga mabao 23, wamefungwa mabao 29, wanapointi 25.


Mechi nyingine Namungo ndio timu iliyocheza mechi chache 18, wapo nafasi ya kumi, wameshinda mechi saba, wametoka sare sita, wamefungwa tano, wamefunga mabao 15, wamefungwa mabao 15 pointi zao ni 27.


Wakati wapinzani wao Ihefu wapo nafasi ya 17, timu ya pili kutoka mkiani wakiwa wamecheza mechi 24, wameshinda tano, wametoka sare tano, wamefungwa 14, wamefunga mabao 14, wamefungwa mabao 34, wamekusanya pointi 20. 


Kocha wa Namungo, Hemed Morocco amesema kama watashinda mechi zake za viporo zote maana yake watakusanya pointi ambazo zitawapeleka katika timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi.


"Tunataka kushinda mechi nyingi zilizokuwa mbele yetu ikiwemo hii dhidi ya Ihefu ingawa tunatambua si rahisi kupata matokeo mazuri dhidi ya timu ambayo ipo katika nafasi ya chini katika msimamo wa ligi," amesema Morocco.


Kocha wa Ihefu, Zubery Katwila naye amesisitiza kwa kusema; "Bado tupo katika mapambano ya kuipigania timu kupata matokeo mazuri malengo makubwa ni kuibakisha katika ligi msimu huu."