Julio akoleza mzuka Morocco

Muktasari:
Mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku kwa saa za hapa ambazo ni sawa na saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania na Kihwelo ametamba anaona Simba ikiandika historia katika hatua hiyo.
KOCHA Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ni miongoni wa Wanasimba walioambatana na timu hiyo kuja hapa Morocco na kukoleza mzuka kabla ya mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, Jumamosi ijayo na kama kawaida yake amekoleza mzuka kwa kuhamasisha mastaa.
Mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku kwa saa za hapa ambazo ni sawa na saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania na Kihwelo ametamba anaona Simba ikiandika historia katika hatua hiyo.
Julio, alisema kwa maandalizi ambayo yanaendelea kufanywa na Simba yanampa matumaini timu hiyo itafanya vizuri katika mechi dhidi ya Berkane, licha ya kucheza ugenini.
“Mechi ya fainali sio rahisi kwetu Simba, kwa sababu tunacheza na timu ngumu na itakuwa katika uwanja wa nyumbani lakini kwa haya maandalizi ninayoyaona, nina imani mambo yatakuwa mazuri,” alisema Julio aliyewahi kuwika na timu hiyo miaka ya 1990 kabla ya kuinoa kwa vipindi tofauti baadae.
“Mechi hii ya kwanza huku ugenini ndiyo muhimu zaidi kupata matokeo mazuri ili kazi tukaimalizie nyumbani,” alisema Julio akiwahamasisha wachezaji kupambana kwa dakika 90 za mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Mji wa Berkane.
Julio alisema wachezaji wanapaswa kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa mashindano hayo msimu huu ili kufuta historia mbaya ya timu hiyo kukosa Kombe la CAF mwaka 1993 baada ya kupoteza ikiwa nyumbani kwa mabao 2-0 licha ya awali kutoka suluhu ugenini dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.