Julio aishangaa Simba, ampa tano Ayoub

Muktasari:
- Pia mkongwe huyo aliyewahi kukipiga CDA na Pilsner, alisema hata kelele zinazopigwa kwa kipa mpya kutoka Morocco, Ayoub Lakred ni kuonyesha wadau wengi wa soka ni ‘oyaa oyaa’, bila kuangalia kiufundi na akasema huyo ni kipa mzuri akitaka apewe muda ili awazibe midomo wanaombeza.
BEKI na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amekiangalia kikosi cha sasa cha timu hiyo na kusema anashangazwa namna mashabiki na wapenzi wa soka nchini wanavyokibeza wakitaka kiendane na kasi ya Yanga, akisema timu hiyo ni bora, lakini inahitaji muda ili kuimarika zaidi.
Pia mkongwe huyo aliyewahi kukipiga CDA na Pilsner, alisema hata kelele zinazopigwa kwa kipa mpya kutoka Morocco, Ayoub Lakred ni kuonyesha wadau wengi wa soka ni ‘oyaa oyaa’, bila kuangalia kiufundi na akasema huyo ni kipa mzuri akitaka apewe muda ili awazibe midomo wanaombeza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Julio alisema Simba ina kikosi kizuri, ila bado hakijaanza kuelewana hivyo wanahitaji muda zaidi ili kuwa sawa na kutuma salama kwa mashabiki na wapenzi kuwa na subira.
“Mafanikio ya misimu minne iliyoyapata Simba ndio yanayowatesa wengi, lakini hawaangalii kama timu hiyo imekuwa na mabadiliko ilikuwa na Luis Miquissone na Clatous Chama wakaondoka ikavunja utawala wamerudi lakini bado hawapo katika mfumo,” alisema Julio.
“Mfano Yanga ina mafanikio makubwa misimu hii miwili kwa vile ilijitafuta na kujipata. Kwa wanaokumbuka ilimsajili Joyce Lomalisa kila mmoja alikuwa anambeza wakiwemo wana Yanga wenyewe lakini sasa ni mchezaji mzuri na anaisaidia timu.”
Julio alisema Simba ipo vizuri na ina kikosi kizuri kilichopo sasa ni namna ya kuitengeneza ili iweze kuwa na muunganiko mzuiri na wachezaji kuelewana.
“Sare yao dhidi ya Power Dynamos isiwatoe mchezoni bado ina nafasi ya kufanya vizuri nyumbani na kutinga makundi kuhusu kikosi chao ni kizuri waachane na maneno wazingatie kujijenga zaiidi kama ilivyokiwa kwa Yanga ambayo sasa imejipata na imekuwa bora,” alisema Julio aliyewahi pia kuzinoa timu mbalimbali hapa nchini.
“Hata mtoto anaanza kukaa kutambaa na baadae kutembea hakuna mtu anazaliwa na kutembea Simba wamevunja kikosi chao wamesajili wachezaji wengi wanahitaji muda kujipata, ukiangalia Yanga msimu huu wameboresha maeneo timu ilikuwa imekamilika na waliowaongeza wameshaingia kwenye mfumo.”
KIPA AYOUB
Wakati huohuo akimzungumzia kipa Ayoub Lakred kuwa makosa aliyofanya Zambia, alisema hapaswi kuhukumiwa kwani hata makipa bora duniani wanafungwa mabao ya kizembe.
“Ni kipa mzuri ameweza kucheza mashindano makubwa, kwa mafanikio akiwa Morocco apewe muda ataonyesha ubora wake makosa ya mchezo mmoja hastahili kubezwa. Kacheza FAR Rabat ameitumikia kwenye ligi na mashindano ya kimataifa kwanini abezwe kwa mechi moja tu mbona jana (juzi) na Coastal alicheza vizuri? Nina imani naye atakuja kuwa kipa mzuri hapo baadae akiendelea kuaminiwa,” alisema Julio.