Job ampoteza mazima Yondani

NI kama beki mzawa Dickson Job amewasahaulisha mashabiki wa soka nchini pengo la Kelvin Yondani katika kikosi cha Yanga na Taifa Stars baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika mechi zote alizoichezea timu hizo.

Yanga iliachana na Yondani mwaka 2019 na kumsajili Job kutoka Mtibwa Sugar na kutokakana na kiwnago kikubwa anachoendelea kukionyesha uwanjani vimezima kelele zote za mashabiki ambao jina la Yondani lilikuwa bado midomoni mwao.

Job hajaziba pengo la Yondani katika kikosi cha Yanga tu lakini hata katika kikosi cha Stars kwani ameendelea kuonyesha ubora mkubwa kila anapopangwa.

Mwanaspoti limezungumza na wadau mbalimbali wa soka, ambao wamefunguka namna Job alivyoziba pengo la Yondani, aliyeichezea Yanga kuanziaa mwaka 2012 hadi 2019.

Straika wa zamani, Edibily Lunyamila alisema; “Ndio maana hazisikiki kelele za Yondani kwa sasa, kwasababu Job anacheza mipira ya aina yote pale nyuma, mirefu, mifupi, anaanzisha mashambulizi, ana uwezo wa kucheza na mchezaji wa aina yoyote, akiendelea hivyo namuona mbali sana, ameweza kuendana na mazingira ya Yanga kwa uharaka, anapambana na kuonyesha kiwango.”

Aliyekuwa beki wa kati wa Simba, Kasongo Athuman alisema licha ya kwamba haishabikii Yanga, lakini anafurahishwa na kazi anayoifanya Job. Mkongwe, George Masatu alisema japokuwa hajamfuatilia kiundani Job baada ya kujiunga na Yanga, ila kama ana muendelezo wa kile alichokuwa anakifanya akiwa Mtibwa Sugar, atakuwa tegemeo kwa timu yake na Stars.