JKT, Yanga zawahi Isamuyo, mechi hatihati kuchezwa

Muktasari:

  • Mchezo huo umepangwa kufanyika leo kuanzia saa 10:00 jioni na Mwanaspoti lililofika mapema kwenye uwanja huo limeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwa pembezoni mwa uwanja kusubiri majibu ya mkaguzi kama mchezo huo utaweza kuchezwa kutokana na hali ya mvua inayoendelea.

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya JKT Tanzania na Yanga huenda usifanyike kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo kutokana na kujaa maji kutokana na mvua, licha ya juhudi za kuyaondoa kuendelea kufanyika.

Mchezo huo umepangwa kufanyika leo kuanzia saa 10:00 jioni na Mwanaspoti lililofika mapema kwenye uwanja huo limeshuhudia viongozi mbalimbali wakiwa pembezoni mwa uwanja kusubiri majibu ya mkaguzi kama mchezo huo utaweza kuchezwa kutokana na hali ya mvua inayoendelea.

Utaratibu unaofanyika ni wa kufyonza maji kwa kutumia magodoro na kukausha, ingawa hali bado sio nzuri, kwani manyunyu ya mvua yanaendelea na kusababisha maji kuendelea kutuama kwenye baadhi ya maeneo ya uwanja.

Eneo linaloonekana kuwa na maji ni katikati ya uwanja na kuna mashimo madogo yanayosababisha maji kutuama.

Wakati huo huo, kwa upande wa mashabiki hawajajitokeza kwa wingi huku muda ukizidi kwenda na hadi saa 8:30 idadi ilikuwa ndogo.

Wakati huo huo, vikosi vya timu hizo zimepishana kuingia uwanjani hapo kwa dakika tatu na kuingia moja kwa moja kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

JKT ndio ilikuwa ya kwanza kuwasili uwanjani hapo saa 8:30 kabla ya dakika tatu baadaye Yanga kuingia.

Yanga inaingia uwanjani kusaka pointi tatu ili kuongeza gepu la ushindani kuwania ubingwa dhidi ya Azam FC na Simba.

Yanga ikishinda leo itafikisha pointi 61 na itabakiza mechi nne tu ili kutetea taji lao walilolibeba msimu uliopita.

JKT Tanzania inasaka pointi tatu kutafuta uhakika wa kucheza tena Ligi msimu ujao na ipo nafasi ya 15 na pointi 22, baada ya michezo 22.