JKT Tanzania yagomea kucheza Chamazi

Muktasari:

  • Habari zinasema, endapo mvua zitaendelea kunyesha, JKT Tanzania italazimika kutafuta uwanja mwingine kwa ajili ya mechi zao za nyumbani, hivyo wamepanga kwenda Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha au Jamhuri pale Dodoma na siyo Azam Complex.

WAKATI Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ukishindwa kutumika kwenye mechi ya Ligi Kuu kati ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga, kutokana na sehemu ya kuchezea kujaa maji, habari za ndani ni timu ya nyumbani ambayo ni JKT Tanzania imekataa kucheza Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Habari zinasema, endapo mvua zitaendelea kunyesha, JKT Tanzania italazimika kutafuta uwanja mwingine kwa ajili ya mechi zao za nyumbani, hivyo wamepanga kwenda Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Arusha au Jamhuri pale Dodoma na siyo Azam Complex.

Sakata la Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, linatukumbusha Januari 09, mwaka huu mechi ya Ligi Kuu Wanawake kati ya JKT Queens na Simba Queens iliyotakiwa kupigwa Uwanja wa Azam Complex, JKT iligomea ikisema inajua mchezo huo ambao wao walikuwa wenyeji, unapigwa uwanja wao wa nyumbani wa Jenerali Isamuhyo, jambo lililowafanya kupigwa faini na kupokonywa pointi.

UAMUZI WA MCHEZO
Kamishina wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya JKT Tanzania dhidi ya Yanga uliopangwa kuchezwa Aprili 23, 2024 kwenye uwanja huo, Kamwanga Tambwe amesema baada ya kujiridhisha wamegundua uwanja huo umejaa maji, hivyo mchezo hauwezi kuchezwa.

Taarifa rasmi zitatolewa baadaye ni lini mchezo huo utachezwa na ni uwanja gani, hivyo wanaenda kuwasiliana na viongozi wa juu.

Tambwe amesema: "Kwa mujibu wa kanuni za ligi, ikiwa mchezo haujachezwa hata sekunde moja, unaweza kupangiwa siku nyingine tofauti kuanzia kesho yake, lakini ungekuwa umechezwa hata kwa dakika moja, basi lazima ungechezwa siku inayofuata."

YANGA WABAKI KUFANYA MAZOEZI, WATIMULIWA
Baada ya mchezo huo kuahirishwa, wachezaji wa Yanga waliendelea kufanya mazoezi mepesi chini ya kocha msaidizi, lakini msimamizi wa uwanja huo, Sajenti Ashiraf Said akawataka waondoke, huku ikielezwa sababu za kuwaambia waondoke ni mchezo kuahirishwa kutokana na uwanja kutokuwa katika hali nzuri, hivyo hakuna ruhusa ya kufanya mazoezi.