JKT Tanzania wakomaa na vijana

Muktasari:

  • JKT Tanzania ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Championship msimu uliopita

Uongozi wa JKT Tanzania FC umepanga kufanya uwekezaji mkubwa kwa timu zao za vijana ili zitumike kuibua na kuzalisha wachezaji ambao watatumika katika timu yao ya wakubwa inayoshiriki Ligi ya Championship.

Katibu Mkuu wa timu ya JKT Tanzania, Abdul Nyumba amesema kuwa mpango huo unalenga kuwa na wachezaji wasiopungua 50 katika timu yao ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na ile ya chini ya umri wa miaka 20 ambao baadhi watakuwa wanapandishwa katika kikosi cha wakubwa.

"Kwa sasa tupo katika mchujo wa mwisho wa kupata wachezaji ambao wataingia katika timu zetu za vijana kuungana na wale ambao tayari wapo ambapo kwa timu ya U17 tunatarajia kupata wachezaji 25 na kwenye kikosi cha U20 pia wataingia wachezaji 25."

"Lengo la hili ni kutengeneza na kuwaandaa wachezaji ambao ndio tutawatumia katika kikosi cha timu yetu ya wakubwa ya JKT Tanzania hivyo ni mpango wa muda mrefu ambao Jeshi linao katika juhudi za kuleta maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania," alisema Nyumba.

Kwa mujibu wa Nyumba, mpango huo umepewa baraka zote na Jeshi la Kujenga Taifa ambalo ndio linamiliki timu hiyo.

"Tunaushukuru uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa chini ya Afande Meja Jenerali Rajabu Mabele kwa kusapoti mpango huu. Lakini pia tunawashukuru wazazi ambao wameonyesha muitikio mkubwa wa kuleta watoto wao kwa ajili ya kufanya majaribio."

"JKT ipo kwa ajili ya kulea na kuwajengea vijana uzalendo hivyo kupitia mpira wa miguu tunaamini tunaweza kulitimiza hili kupitia mpango huu," alisema Nyumba.