JKT Quuens mabingwa Ligi Kuu Wanawake

Dar es Salaam. Maafande wa JKT Queens hawakamatiki hata kidogo kwani kwa pointi 36 walizofikisha, tayari wametangaza ubingwa kwenye michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu.

JKT Queens imetangaza ubingwa huo kwa sababu pointi ambazo walizopata katika mechi 12, hazitafikiwa na timu nyingine yeyote.

Timu hiyo inayomilikiwa na jeshi, imekuwa tishio tangu michuano hiyo ianze kwani haijapoteza hata mchezo mmoja na kufunga mabao 51.Kutokana na mafanikio hayo, JKT Queens imewavua ubingwa Mlandizi Queens waliotwaa msimu uliopita.

Kocha wa timu hiyo, Ali Ali amesema baada ya kujihakikishia ubingwa huo, wanachofanya ni kulinda heshima ya kutofungwa katika mechi mbili zilizosalia.

"Hatutaki kuchafua rekodi yetu, tumejipanga kuhakikisha tunamaliza kwa kishindo licha ya kubakiwa na mechi ngumu na timu zenye ushindani ambazo ni Kigoma na Mlandizi, lakini lazima tufikie malengo yetu,"alisema.

Kigoma ndiyo wanaifuatia JKT Queens kwa  pointi 27 baada ya kucheza mechi 12, imeshinda michezo tisa na kupoteza mitatu, lakini nahodha wa timu hiyo, Amina Ally amesema ilikuwa safari ndefu kwao kwa kuwa ligi ilikuwa inasimama simama.

"Tumebakiza mechi mbili dhidi ya JKT Queens ambayo tayari imekuwa mabingwa na mechi ya mwisho itakuwa dhidi ya Evergreen,kikubwa TFF waboreshe ratiba na kusaka wadhamini zaidi ili soka la wanawake liweze kuwa na manufaa kwa wachezaji,"alisema.