JKT Queens kuifuata Mamelodi kesho

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake, JKT Queens itaondoka kesho nchini kwenda jijini Abdijan nchini Ivory Coast.

JKT inashiriki michuano hiyo baada ya kuwa bingwa wa CECAFA kwa kuifunga C.B.E ya Ethiopia mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya bila kufungana.

Hii inakuwa mara ya pili kwa timu kutoka Tanzania kushiriki michuano hiyo baada ya msimu uliopita Simba Queens kuchukua ubingwa wa CECAFA na kuishia nusu fainali CAF.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire amesema timu hiyo itasafiri kesho Novemba Mosi saa 10 alfajiri kwenda Abdijan, Ivory Coast ikiwa na wachezaji 21 na viongozi saba.

Masau alisema wachezaji 16 ambao wanaitumikia timu ya taifa 'Twiga Stars' watajiunga na timu Novemba 02.

"Malengo yetu ni kufika fainali na kuleta kikombe nyumbani, tunaamini uwezo wa wachezaji wetu na kesho timu inaondoka kwenda Ivory Coast, wengine waliokuwa timu ya taifa watajiunga na timu Novemba 02," alisema Masau

Michuano hiyo inaanza Novemba 05 mwaka huu na JKT itaanza na Mamelodi Sundown Ladies saa 5 usiku ikiwa mwenyeji kisha Novemba 08 saa 2 usiku na Atlentico Abidjan ya Ivory Coast na kumaliza na SC Casablanca ya Morocco Novemba 11 hatua ya makundi ambapo timu hiyo imepangwa kundi A.