JKT Queens kimataifa

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Ukanda wa Cecafa, JKT Queens wanaondoka leo nchini kwenda Abdijan Ivory Coast huku wakiwa na matumaini kibao ya kutwaa ubingwa huo.

JKT inashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa wa CECAFA ikiitoa C.B.E ya Ethiopia kwa penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Hii inakuwa mara ya pili kwa timu za Tanzania kushiriki michuano hiyo baada ya msimu uliopita Simba Queens kuchukua ubingwa wa CECAFA na kuishia nusu fainali CAF.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire alisema timu hiyo ilianza safari leo saa 10 alfajiri ikiwa na wachezaji 21 pamoja na viongozi saba.

Masau alisema wachezaji 16 ambao wanaitumikia timu ya taifa ‘Twiga Stars’ watajiunga moja kwa moja na timu kesho Alhamis.

“Malengo yetu ni kufika fainali na kuleta kikombe nyumbani, tunaamini uwezo wa wachezaji wetu na leo timu inaondoka kwenda Abdijan Ivory Coast wengine waliokuwa timu ya taifa watajiunga na timu Novemba 2,” alisema Masau.

Msimu huu michuano hiyo itafanyika Ivory Coast na timu nane zitashiriki kutoka ukanda tofauti ikiwemo As FAR ya Morocco, Ampem Darkoa (Ghana), Huracanes FC (Equatorial Guinea) na AS Mande (Mali) zikiwa zimepangwa kundi B.