JIWE LA SIKU: Ule ubabe wa Yanga, Simba ndio huu sasa!

JUZI nilibahatika kutembelea makao makuu ya klabu ya Yanga baada ya kupita miaka kadhaa. Nilichokiona katika mitaa ya Twiga na Jangwani kilibadilisha mtazamo wangu kuhusu hatua iliyopigwa na klabu hiyo kongwe. Ikumbukwe juma lililopita Yanga ilikuwa kwenye shamrashamra za kufikisha miaka 89 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1935 huku ndugu zao Simba watafikisha umri huo mwakani na miaka miwili ijayo wote watakuwa na 90 na zaidi.

Niliona mabadiliko mengi ndani ya jengo la klabu ya Yanga pale Jangwani, jengo hili, kwa mujibu wa bango lililoko nje, lilizinduliwa mwaka 1971 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheikh Abeid Aman Karume.

Sheikh Karume ndiye aliyesaidia klabu za Yanga na Simba kwa fedha za kujenga makao makuu yao Jangwani na Msimbazi hivyo naamini wazee wachache waliokuwepo mwaka 1971 hadi leo watafurahi wakiingia ndani ya jengo hilo na kuona mabadiliko.
Nilipofika ndani ya klabu hiyo nilikuta sehemu ya mapokezi iliyobadilika kwa kiasi kikubwa ikiwa imenakishiwa na vikombe ambavyo vilinyakuliwa katika mashindano mbalimbali ya ndani na ya kimataifa huku vingi vikiwa vile vilivyochukuliwa miaka 2000 na kuendelea.

Nilihoji viko wapi vikombe vingine? Nikaambiwa miaka ya nyuma vikombe na mali nyingine za klabu ziliwekwa nyumbani kwa viongozi na klabu zaidi ilikuwa mahali pa wanachama kupiga gumzo au mara nyingine kama sehemu ya kulala wachezaji hivyo kuna baadhi havikuweza kurudi.

Ndani ya jengo la klabu hiyo kuna chumba cha habari (media room) cha hadhi ya kisasa kabisa ambamo waandishi wanaweza kukutana na kufanya vikao na kazi zao bila shida.
Wakuu wa idara mbalimbali kama mashindano, wanachama, ufundi, masoko na habari wana ofisi ndani ya jengo hilo na kwa ujumla shughuli zote za sekretarieti na timu ya Yanga zinaweza kufanyika ofisini kwao bila kukwama.

Ninaweza kusema dhahiri kwamba ukarabati uliofanyika ndani ya jengo la Yanga unaifanya ofisi yao kuwa moja ya ofisi bora za klabu barani Afrika nilizowahi kuzitembelea.
Mgeni anapofika ndani ya jengo hilo atakubali kwamba yuko ndani ya taasisi yenye mafanikio na mipango mikubwa na endelevu.

Katika mipango yao endelevu ambayo matokeo yake yanaweza kuonekana ni pamoja na mifumo mbalimbali ya kuingiza wanachama wa klabu kama kadi za uanachama zimefungamanishwa na kadi za benki kama CRDB na NMB katika mikataba ya kibiashara.

Pia uanachama wa klabu hiyo umeunganishwa na huduma za kijamii kama mkataba mpya walioingia na hospitali za Aga Khan ambako wanachama watapata nafuu katika gharama za matibabu kwenye hospitali zilizo chini ya hospitali ya Aga Khan.

Hii inaonyesha namna thamani ya idadi kubwa ya wapenzi na wanachama inaweza kubadilishwa na kuwa chanzo cha mapato kwa klabu.

Klabu ina wadhamini wa aina mbalimbali kuanzia kampuni na taasisi zinazotoa huduma kama Aga Khan, NMB na CRDB, zile zinazouza bidhaa kama GSM na Haier na pia zile za matangazo ya redio na televisheni kama Azam Media na wengine zaidi.
Kwa miaka mingi huku Afrika chini ya jangwa la Sahara ukiondoa Afrika Kusini, ilikuwa ni shida kweli kuona klabu ina wadhamini zaidi ya wawili.

Mara nyingi klabu zilitegemea michango ya wafadhili ili kuweza kuendesha mambo yao na haikuwa tofauti kwa Yanga kwani ufadhili ulikuwa ni chanzo kikubwa cha mapato lakini kwa kinachoendelea sasa, uwekezaji unakwenda kuchukua nafasi ya ufadhili.

Na wafanyabiashara hawawekezi tu, wanajua namna watakavyofaidika kwa kujihusisha na chapa ya Yanga ambayo ni taasisi iliyodumu kwa miaka 90 inaweza kukupa kile unachotaka bila kujali ni wa kizazi gani kwani ni chapa ya kizazi cha sasa, kilichopo na kijacho.

Mara nyingi kumekuwa na kauli za kubeza mafanikio ya Yanga na Simba katika medani ya mpira wa miguu. Ni kweli siwezi kusema hakuna upungufu lakini ziko taasisi ngapi za umma, ukiondoa za dini, hapa nchini ambazo zimeweza kudumu na kubaki na utambulisho wao kwa muda mrefu kiasi hiki?
Ziko klabu ngapi za namna hii hapa Tanzania na Afrika Mashariki? Ni klabu ngapi zimehimili mawimbi na misukosuko kwa miongo mingi? Labda katika Ligi ya Tanzania Bara unaweza kuitaja Coastal Union ya Tanga iliyoanzishwa mwaka 1948 kuwa klabu inayofuatia katika nafasi ya 3 kwa umri ambayo muda mwingi imecheza katika daraja la juu.

Timu kama Pan African, Cosmopolitan, Dar Cargo, Mwadui, Pamba United, CDA na nyingine nyingi zimekufa au kama zipo zinatokeza kwa 'kubipu'.

Ukiangalia timu zilizoko Ligi Kuu na ulinganishe na Yanga na Simba utaona kuwa ni vijana dhidi ya wazee na wazee ndio wanafanya vizuri.

Hii ni changamoto kwa klabu nyingine katika kutafuta na mafanikio na kuwa endelevu kama nilivyosema awali, Yanga na Simba zinaweza kuwa hazijafikia malengo ambayo ni ndoto yao lakini zinaweza kufikia hata kupita malengo ya waasisi yao.

Pia ni muhimu kujua, taasisi kama ilivyo kwa viumbe vyote vyenye uhai hukua kufuatana na changamoto za ndani na za mazingira pia.

Klabu za Yanga na Simba zimekuwa zikibadilika kadri mazingira ya uendeshaji wa klabu yanavyobadilika, kwa mfano, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) lilipoanzisha utekelezaji wa kanuni za shirikisho la mpira Afrika (CAF) kuhusu leseni za klabu.

Klabu hizi zilibadilika ili kuendana na matakwa ya CAF kama kuwa na sekretarieti ya kuajiriwa, taarifa za fedha n.k.
Bado kuna upungufu kwa mfano wa kutokuwa na viwanja (stadiums) vinavyomilikiwa na klabu hizo lakini kama nilivyosema awali, mazingira yanaamua nini kinahitajika haraka.

Klabu za Yanga na Simba zimekuwa wamiliki wa viwanja vya Dar es Salaam kama Ilala (Karume), Taifa (Uhuru) na Taifa (Benjamin Mkapa).

Naamini kabisa uwepo wa viwanja hivi, ulichangia kwa kiasi kikubwa kwa klabu hizi kubweteka kwani hazijawahi kukosa sehemu ya kuchezea mechi zao ingawa hata hivyo Yanga imetangaza kuanza ujenzi wa uwanja wao (Stadium) pale Jangwani.

Ikiwa jaribio hili halitakuwa kama majaribio yaliyokwama huko nyuma, basi uongozi wa sasa utaingia kwenye vitabu vya historia sawa na kina Dr Jabir Katundu walioweka alama pale Twiga na Jangwani.

Pamoja na kuhitajika miundombinu ya mpira wa miguu ambao ni biashara yao kuu, maendeleo ya vijana ni changamoto kubwa.
Klabu yoyote ya mpira wa miguu mbali na kuchukua vikombe, bado hujivunia kizazi cha vijana inachokilea. Angalia klabu kubwa kama Manchester united, Arsenal, Liverpool na nyingine zilizoko England na huku Afrika kama Ahly na Zamalek za Misri ambazo siku zote hujivunia shule zao za vijana ambazo ziko kwenye rekodi kwa kutoa vipaji vikubwa.

Katika mpira wa miguu, yako mafanikio utayanunua lakini mafanikio mengi yatategemea uwekezaji wa muda mrefu katika vijana.

Nimepitisha macho katika orodha ya klabu kongwe za mpira wa miguu duniani na nilichogundua nyingi hazina uhai tena au hata kama zinao bado hazina nguvu katika mashindano ya juu ya nchi zao.

Sheffield United ya England, Genoa ya Italia, Le Havre ya Ufaransa na nyingine chache zinaendelea kusimama kama taasisi pamoja na ukongwe wao lakini hawa pia uwepo wao na ushiriki wao kwenye ligi za mataifa yao umekuwa si wa kutisha.
Historia za Yanga na mahasimu wao Simba zinaweza kuwa za aina yake hapa Afrika na duniani pia. Historia ya mchezo wa mpira wa miguu inaanzia kwenye taasisi hasa shuleni, vyuo na hata viwandani.

Kwa timu za mitaani zilizo huru kudumu kwa umri huo na bado zikawa na 'umiliki' wa ligi ya nchi si suala dogo na kitu kingine nilichokiona kwenye jengo hilo kinakupa taswira ya jinsi klabu hizi zimekuwa na unyumbulifu kutoka kizazi hadi kingine.
Ili kupambana na changamoto za wakati huo huku wakikidhi mahitaji ya sasa na yajayo, miaka 11 ijayo haitashangaza kusikia watu wakisherehekea karne (miaka 100) ya mafanikio.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.