JIWE LA SIKU: Tshabalala' miaka 10 Simba kama msimu mmoja

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mwamba huyu hapa. Mohamed Hussein 'Tshabalala'. Nusu mtu nusu mashine. Huenda nyota huyu wa Simba akaonekana wa kawaida kwa macho ya wengi na hii ni kutokana tu na utamaduni uliojengeka kwa mashabiki wa soka hapa nchini kuwa na tabia ya kumchoka mtu hata bila ya sababu za msingi. Lakini muangalie vyema, huyu jamaa ni mashine. Miaka 10 Simba ni kama kacheza msimu mmoja, hachoki, hang'oki.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wapo wachezaji wengi wanaoimbwa ndani ya Simba kutokana na uhodari wao na siku zote wamekuwa ni washambuliaji zaidi bila ya kuangalia nafasi nyingine na mchango wa mtu ingawa kama ulikuwa hufahamu, 'Tshabalala' anastahili kupewa maua yake.

Sababu kubwa ya kusema hivyo ni kutokana na mchango wake ambao amekuwa anautoa ndani ya timu hiyo na sio hapo tu kwani hata kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' amekuwa mchezaji muhimu wa kutegemewa anayetumia miguu yake vizuri.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kuonyesha kama sio mtu wa utani, nyota huyu amekuwa hana mshindani katika kikosi cha Simba hali inayosababisha mastaa mbalimbali wanaosajiliwa ili kushindania naye nafasi wamejikuta wakiondoka au wakisotea benchi kutokana na ubora wake.

'Tshabalala' sio mtu wa kujikweza au kujiona ila anachokifanya ni kuhakikisha nafasi anayopewa uwanjani anaitendea haki bila kujali tofauti na wachezaji wengine ambao wamekuwa wanalewa sifa mapema na kujikuta vipaji vyao vikiyeyuka haraka.

Kwa mara ya kwanza nyota huyu alijiunga na Simba Juni 2014 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba baada ya awali kuchezea pia akademi ya Azam FC.

Kwa sasa ana miaka 10 ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi na amekuwa na ubora ule ule wa kiwango chake licha ya kuletewa wachezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ila walichemka mapema na kumuacha nyota huyo akiendelea kupeta hadi sasa.

Wachezaji walioletwa kikosini Simba wanaocheza nafasi yake ya beki wa kushoto ni wengi na wameshindwa kufurukuta ila tu baadhi yao walikuwa ni, Jamal Mwambeleko aliyesajiliwa na kikosi hicho akiwa na kiwango bora wakati akiitumikia Mbao FC.

Mwambeleko licha ya kiwango bora alichokuwa nacho wakati akiwa na Mbao ya jijini Mwanza ila ujio wake Simba ulikuwa kama kaa la moto kwani alishindwa kupenya kwa 'Tshabalala' na mwishoni aliomba kuondoka na kujiunga zake na Singida United.

Mwingine ni Mghana, Asante Kwasi ambaye naye alionekana huenda akapindua ufalme wa 'Tshabalala' Simba wakati anasajiliwa mwaka 2017 akitokea Lipuli ya Iringa kutokana na ubora wake wa kuzuia na wakati huohuo kuanzisha mashambulizi ya hatari.

Kiukweli, Kwasi alionekana ni mchezaji tishio ingawa naye alijikuta akilewa sifa mapema na mwishoni akashindwa kupigania namba na nyota huyo na baada ya kudumu misimu miwili aliondoka ndani ya kikosi hicho 2019 na kujiunga na klabu ya Hafia ya Guinea.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Maisha yalienda kasi kwa nyota huyo kwani hata huko nchini Guinea alishindwa kuonyesha kiwango kizuri na kujikuta pia akiachwa na kurudi tena Bongo na kujiunga na Kitayosce FC kwa sasa Tabora United wakati inashiriki Ligi ya Championship.

Nyota mwingine aliyeingia kwenye mtego wa 'Tshabalala' ni Gadiel Michael ambaye alijiunga na kikosi cha Simba 2019 akiwa ni chaguo namba moja akitokea Yanga ila mambo yalikuwa magumu kwake na baadaye kuondoka na kujiunga na Singida Fountain Gate.

Kucheza Simba au Yanga na kushindwa kuonyesha kiwango kizuri haina maana huwezi kuonekana kwingine kwani baada ya Gadiel kutua Singida alicheza vizuri sana msimu huu na kupata shavu la kujiunga na Cape Town Spurs FC ya nchini Afrika Kusini.

Hao ni baadhi tu ya wengi walioushindwa 'mziki wa Tshabalala' pale Simba na kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine ili kuokoa vipaji vyao vilivyokuwa vinazidi kudidimia licha ya klabu mbalimbali walizotoka kuonekana wana ubora mzuri.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kuonyesha ubora wa nyota huyo, wakati wachezaji mbalimbali wakipewa mapumziko kutokana na ushiriki wao kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ila kwa upande wa 'Tshabalala' mambo ni tofauti kwake kwani anaendelea kukipiga kama kawaida.

'Tshabalala' alikuwa nchini Ivory Coast katika fainali hizo akiwa na kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' ambacho hata hivyo hakikuweza kufanya vizuri na kutolewa mapema baada ya kuburuza mkia katika kundi 'F' kikiwa na pointi zake mbili.

Baada ya Stars kuondolewa wapo baadhi ya wachezaji walipewa mapumziko kidogo kabla ya kuendelea na michuano mbalimbali ila kwa 'Tshabalala' kutokana na umuhimu wake aliendelea kukipiga huku akianzia benchi mchezo mmoja tu tangu amerudi.

Tangu Stars iondolewe Simba imecheza michezo minne ambapo mitatu kati yake ni ya Ligi Kuu Bara huku mmoja tu ukiwa ni wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 dhidi ya Tembo ambao ndio pekee 'Tshabalala' alioanzia benchi kikosini.

Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda mabao 4-0 na kusonga mbele hatua ya 32 bora, nafasi yake ilichukuliwa na Israel Mwenda ambaye kiasili hucheza beki namba mbili ila baada ya hapo ameendelea kucheza nafasi yake akiwa hana mshindani.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Michezo yote mitatu ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, Tabora United na Azam FC, nyota huyo aliendelea kukiwasha kama kawaida yake tena akionyesha kiwango bora na kuvaa kitambaa cha unahodha kuonyesha ni mchezaji muhimu na mwenye nidhamu.

Huyo ndiye 'Tshabalala', mchezaji asiyezungumzwa sana ila kazi ya miguu yake inaongea zaidi uwanjani na anastahili kupewa 'maua yake'.