JIWE LA SIKU: Kama mlimnyima Mwinyi siri ya Simba 1993 tupeni sisi

Muktasari:

  • Ni miaka 31 sasa tangu pambano lile lichezwe. Wapo wengi waliotangulia mbele za haki. Rafiki zetu kina Ramadhan Lenny, fundi kiungo, Edward Chumilla, mshambuliaji hatari. Wapo wengine waliotangulia mbele za haki. Kina Ally Machela, kina Damian Kimti na wengineo wengi.

Aliyekua mgeni wa rasmi wa pambano la fainali Kombe la CAF kati ya Simba na Stella Abidjan 1993, Mzee Ally Hassan Mwinyi amelazwa katika nyumba yake ya milele Jumamosi hii iliyopita pale katika kijiji cha Mangapwani, Zanzibar. Ni namna nyakati zinavyokwenda kasi.


Ni miaka 31 sasa tangu pambano lile lichezwe. Wapo wengi waliotangulia mbele za haki. Rafiki zetu kina Ramadhan Lenny, fundi kiungo, Edward Chumilla, mshambuliaji hatari. Wapo wengine waliotangulia mbele za haki. Kina Ally Machela, kina Damian Kimti na wengineo wengi.


Ni miaka mingi ya fumbo la ajabu kidogo. Simba ilipotezaje pambano hili la pili la fainali? Pambano ambalo baadaye Mzee wetu Mwinyi akatoa kauli kali kwamba Tanzania ilikuwa kama kichwa cha mwendawazimu lilipokuja suala la soka. Kila mtu (akimaanisha kila nchi) alikuwa anajifunzia kunyoa kwetu.


Ni miaka ya fumbo kwa namna pambano lenyewe lilivyopotezwa. Pambalo la kwanza lilichezwa Abidjan na Simba walifanikiwa kupata suluhu yaani bila kufungana. Ilionekana kuwa nafasi ya dhahabu kwa Simba na Tanzania kwa ujumla kunyanyua kwapa lake la kwanza katika michuano ya kimataifa.


Maandalizi yalikuwa makubwa. Kuna vitenge na fulana zilitengenezwa vikiandikwa ‘Simba bingwa wa CAF 1993’. Wachezaji wa Simba na benchi la ufundi kila mmoja aliahidiwa gari kubwa aina ya KIA. Ukijumlisha idadi ya wachezaji na benchi la ufundi basi KIA 30 zilipaswa kumtoka aliyekuwa tajiri wa Simba enzi hizo, Azim Dewji.


Baadaye Uwanja wa Taifa ukafurika. Mzee Mwinyi akawa mgeni wa heshima katika pambano hilo la kihistoria. Simba walihitaji ushindi wowote ule. Sare ya mabao ingewapa ubingwa Stella kwa sababu wangekuwa na bao la ugenini. Matarajio yote na kila kitu kutoka kwa Simba na Watanzania yalikwenda kuishia mguuni kwa mshambuliaji wa Ivory Coast aliyeitwa Boli Zozo. Alimtungua Mohamed Mwameja mabao mawili katika mguu wake. Ilikuwa jambo la kushangaza.


Wakati huo kutoka suluhu ugenini lilikuwa jambo gumu kwa Simba na timu yoyote ya Tanzania. Ilionekana suala la ushindi wa nyumbani lingekuwa jepesi kwa watu ambao mliwavimbia kwao kwa sare ya bila kufungana. Yote haya yaliishia katika mguu wa Boli Zozo.Mwinyi akakabidhi kombe kwa nahodha wa timu ambayo haikutarajiwa. Badala ya kumkabidhi kombe Ramadhan Lenny yeye akamkabidhi nahodha wa Stella. Hadithi ya matamanio ikaishia hapo. Lakini hapo hapo ndio ukawa mwanzo wa uvumi ambao umedumu kwa miaka 31.


Mgeni rasmi ametangulia mbele ya haki, kuna kundi kubwa la wachezaji na viongozi limetangulia mbele ya haki huku uvumi huu ukishindwa kutoweka. Kwamba kuna baadhi ya wachezaji walihujumu pambano hilo. Kisa? Ahadi ya magari ya KIA ilionekana kuwa ngoma ngumu kwa walioitoa.


Kwamba baadhi ya wachezaji walichotwa na kupewa pesa na viongozi wao ili wapoteze mechi kwa sababu uwezekano wa kumpa kila mchezaji KIA kama wakitwaa ubingwa ulikuwa haupo. Ni uvumi uliodumu mpaka leo.


Kuna wachezaji walishutumiwa. Kama vile kipa Mohamed Mwameja, kiungo Hussein Marsha, beki George Masatu na wengineo. Kuna wakati gazeti hili lilifanya mahojiano na Masatu akadai kwamba walifungwa kikawaida tu kwa sababu walizidiwa mpira.


Lakini kuna wengine ambao wamewahi kufanya mahojiano kwingine na kudai kwamba pambano lilihujumiwa. Kuanzia katika maandalizi hadi kwa namna ambavyo lilichezwa. Wanaamini kwamba Simba walistahili kushinda pambano lile kwa namna yoyote ile.


Tulichokosa na ambacho kinatusikitisha ni kwamba wakati ule mechi hizi zilikuwa hazionyeshwi ‘live’ wala kurekodiwa katika ubora huu ambao Azam TV wanaufanya kwa sasa. Kama ingekuwa hizi sasa hivi tungeweza kukaa mbele ya televisheni zetu na kuchambua makosa yaliyotokea. Yalikuwa ya kibinadamu au kulikuwa na hila?


Lakini hapo hapo tunaweza kukaa kando na kufikiria namna mpira wa sasa ulivyo. Wenzetu walianza zamani sana namna ya kujua jinsi ya kucheza mechi za ugenini na nyumbani. Inawezekana ni kweli hakukuwa na hujuma yoyote ile.


Inawezekana Simba baada ya kutoka sare ugenini waliamua kubweteka na kuona wameshinda mechi. Inawezekana Stella waliwasoma Simba baada ya kukutana nao. Zamani mechi hazikuwa ‘live’ katika televisheni na miundombinu ilikuwa migumu kusafirisha watu ili wakaisome timu pinzani.


Inawezekana baada ya mechi ya kwanza pale Abidjan rafiki zetu Stella waliitumia mechi hiyo kusoma udhaifu wa Simba. Labda wakati huo Simba na Utanzania wetu hatukugundua haya na badala yake tukajihisi tayari tumeshinda nyumbani kwa sababu tumetoka suluhu ugenini.


Vyovyote ilivyo, haya ni mambo ambayo tumeyajua zaidi siku hizi. Labda ndio maana siku hizi vijana wapya katika mpira wameanza kutusogeza mbele katika michuano ya kimataifa. Hata hivyo, haiondoi ukweli wa swali lilelile ambalo Watanzania wengi wanatamani kujua. Nini kilitokea kwa Simba siku ile? Kama kuna wenye ushahidi wa kilichotokea wanaweza kusogea mbele ya kutoa ushahidi wao kabla hawajatangulia mbele za haki.

Katika soka nimemkumbuka zaidi hayati mzee wetu Mwinyi kwa pambano lile. Ilikuwa ni kama vile alikuwa amepigwa na kitu kizito usoni baada ya Boli Zozo kuifungia Stella mabao mawili na kupeleka kombe Abidjan. Inawezekana kuna ukweli ambao alipaswa kuujua baada ya pambano hilo kukamilika.


Hata hivyo, faraja pekee ambayo inabakia ni kwamba mwaka huo huo Yanga walichukua kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki kule Uganda, halafu mwaka mmoja uliofuatia, Taifa Stars walitwaa Kombe la Chalenji kule Nairobi na nahodha Hussein Marsha pamoja na wenzake walipeleka kombe Ikulu na kupokewa na Rais mwenyewe. Vinginevyo pambano la mwaka 1993 linabakia kuwa siri nzito miongoni mwa watu wachache.

Kama hakuna siri yoyote bado ambao wanapaswa kulitetea jambo hili hawajatoa maelezo ya kutosha ya kiufundi na kisayansi ya kwanini Simba walipoteza pambano lile.