JIWE LA SIKU: Jina letu sio safi kimataifa

Muktasari:

  • Kufanyika uzinduzi wa mashindano ya kihistoria ya African Football League (AFL) ni moja ya faida ya kung’aa kwa nyota ya Tanzania kimataifa.

Tanzania tumejitahidi sana kuliuza jina letu kimataifa na kuwa moja ya majina yanayozungumzwa vizuri sana linapokuja suala la soka.


Kufanyika uzinduzi wa mashindano ya kihistoria ya African Football League (AFL) ni moja ya faida ya kung’aa kwa nyota ya Tanzania kimataifa.


Usisahau mwaka 2017, kongamano kuu la mwaka la FIFA lilifanyika hapa nchini na ujio wa AFCON 2027 ni muendelezo wa ubora wa jina la Tanzania.


Lakini hata hivyo, jina hili zuri la Tanzania linachafuliwa kwa kiasi kikubwa sana na tuhuma za hujuma za nje ya uwanja katika mechi za kimataifa za vilabu vyetu vya hapa nchini.


Tangu Simba wafungue milango ya Tanzania kimataifa msimu wa 2018-2019, hali ni mbaya hadi sasa.
Mechi ya mwisho ya hatua ya makundi kati ya Simba na AS Vita ya DRC iliyoisha kwa ushindi wa 2-1 wa Simba kwa bao la jioni la Clatous Chama, ndio ilikuwa mwanzo wa tuhuma hizi.  


AS Vita walilalamika waliwekewa dawa za kupunguza nguvu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Kuanzia hapo ukawa utamaduni wa timu kulalamikia hilo kila zinapokuja nchini.


Hata Namungo walipocheza na C.D. Primeiro de Agosto ya Angola katika mechi za mtoano wa mwisho kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2019-2020, kelele zilikuwa hizo kwa Waangola, baada ya kufungwa 6-2 katika mchezo wa kwanza.


Hata walipoingia hatua ya makundi, timu kadhaa zilikalamikia hujuma, wakiwemo Raja Casablanca ya Morcco  ambao walidai kuwekewa upupu kwenye jezi zao.


Red Arrows ya Zambia ilipocheza na Simba kwenye mechi za mtoano kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, habari ilikuwa hiyo hiyo walilalamikia hadi kuwekewa sumu kwenye chakula.


Al Akhdar ya Libya ilipokuja kucheza na Azam FC hali ilikuwa hivyo hivyo. Rivers United ya Nigeria ilipocheza na Yanga kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho, hali ilikuwa hiyo hiyo.
Tena sio tu dawa, walilalamikia hadi kufanyiwa fujo na kuibiwa vitu vyao wakiwa mazoezini.


Hii ilisababisha hadi CAF kuchukua hatua kali dhidi ya Yanga na kuiweka Tanzania chini ya uangalizi mkubwa.
Msimu huu, Jwaneng Galaxy kutoka Botswana pia wamekalamikia hali hiyo.


Mbaya zaidi kauli iliyotolewa na Waziri wa Michezo, Dk Damas Ndumbaro, ilichafua zaidi hali ya hewa. Hii ikafanya Afrika iamini kwamba ‘uchafu’€  wote unaofanyika Tanzania unajulikana na vyombo vya maamuzi kumbe siyo uhalisia.


Haya yote yamesababisha Tanzania ivume vibaya kwa timu za kigeni kuja kucheza hapa.Ndio maana unaona Al Ahly wamekuja na kila kitu chao kuhakikisha hawaathiriki na hujuma za aina yoyote.


Kocha wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Rhulani Mokwena, akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa Tanzania, Fadhil Omary Sizya, baada ya mchezo wa hatua ya 16 Bora ya Kombe la NedBank alisema; “Unaona hapa kwetu tulivyo wakarimu, hakuna vurugu wala hujuma. Tunajua stori zenu.”€
Hii maana yake ni kwamba picha waliyonayo kuhusu Tanzania ni vurugu na hujuma.


Hii sio picha nzuri kwa jina la Tanzania ambalo lilijengwa katika kutoa matumaini kwa waliokata tamaa.
Wakati timu zetu za Simba na Yanga zikiwa kwenye mechi zao za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kila kinachoweza kufanyika basi na kifanyike ili kusafisha jina zuri la nchi yetu.