JICHO LA MWEWE : Mo Rashid, Kaheza jicho katika pesa, jicho benchi
Muktasari:
- Mchezaji wa kwanza aliyeniachia maswali alikuwa Marcel Kaheza. Alikuwa anakwenda kucheza nafasi ya nani Msimbazi? Nilijiuliza na sikuwa na jibu la uhakika. Nilipenda uchezaji wake akiwa na Majimaji ya Songea. Nilipenda kumtazama.
SIMBA ilipokuwa inatengeneza kikosi cha kukomoa, cha kufikirika, cha kuonyesha watu cha mtema kuni, nilijua kutakuwa na wahanga wa vipaji. Ndiyo, wangekuwepo. Ni kitu cha kawaida katika soka na wakati mwingine hauwezi kuwalaumu wahanga, wala kuilaumu Simba.
Mchezaji wa kwanza aliyeniachia maswali alikuwa Marcel Kaheza. Alikuwa anakwenda kucheza nafasi ya nani Msimbazi? Nilijiuliza na sikuwa na jibu la uhakika. Nilipenda uchezaji wake akiwa na Majimaji ya Songea. Nilipenda kumtazama.
Mwingine ni mwenzake anayesugua naye benchi. Mohamed Rashid. Nilikuwa napenda kusikia amefunga kila siku akiwa na Prisons. Sikuwa na uhakika ni wapi angecheza. Sababu ilikuwa rahisi. Simba ina Emmanuel Okwi, Meddy Kagere, John Bocco na Shiza Kichuya.
Hao wachezaji wanatosha sana kwa Simba kwa sababu moja kuu. Okwi na Kichuya wanaweza kucheza katikati na pembeni. Bocco na Kagere wanaweza kucheza katikati. Wenyewe peke yao wametosha kiasi cha kuwekana benchi kwa sababu kiasili zinahitajika nafasi tatu tu katika mfumo maarufu wa kisasa wa 4-3-3.
Kama mmojawao anakaa nje ina maana anakwenda kuungana na Adam Salamba katika benchi. Iko wapi nafasi ya Kaheza na Rashid? Mungu anajua. Wakati mwingine tatizo sio uwezo wao. Tatizo ni majina makubwa yaliyotangulia mbele yao.
Kuna uongo mwingi huwa unasambaa wakati wachezaji wazuri kama wao wanaposugua benchi. Utaambiwa michuano ipo mingi. Huu ni uongo wa mchana katika soka letu. Sisi tuna michuano mitatu tu. Ligi yetu ya ndani, michuano ya CAF na Kombe la FA.
Kwa Waingereza hapo ungeongeza michuano ya Kombe la Ligi maarufu kama Carabao. Katika michuano yetu, ligi na michuano ya CAF huchezwa na wachezaji muhimu. Kombe la FA linategemea na uzito wa adui. Ikiangukia Simba na Singida United au na Yanga au na Azam FC, usitegemee kuwaona Kaheza na Rashid wakianza. Labda ikiangukia na Newala United.
Lakini hapohapo wachezaji muhimu katika vikosi vya wakubwa wetu huwa hawachezi mechi nyingi za kimataifa. Baada ya kuitoa timu kutoka Shelisheli utapangiwa na Al Ahly ya Misri. Huo ndio unakuwa mwisho wa safari. Ina maana wachezaji wakubwa katika timu kubwa huwa wanacheza mechi nne tu za kimataifa.
Ni nadra sana kwao kucheza mechi nyingi. Inatokea pale wanapofuzu katika hatua ya makundi kama ilivyotokea kwa Yanga msimu uliopita. Vinginevyo mastaa wetu hawawezi kukuachia nafasi kirahisi kwa sababu hawana mechi nyingi kama watu wanavyosema.
Lakini pia katika ligi mahitaji ya Simba na Yanga ni makubwa. Hakuna shabiki wala kiongozi anayekubali Kagere akae nje halafu acheze Mohamed Rashid. Hapo hapo ni kama pia katika benchi kuna Bocco pia. Tunajua matusi ya majukwaa yetu.
Lakini hata katika hali halisi, sidhani kama mechi zetu 38 zinaweza kumpumzisha mchezaji ambaye hana mechi nyingi za kimataifa. Ikumbukwe wachezaji kadiri wanavyocheza mechi nyingi ndivyo wanavyokuwa fiti. Tusijidanganye sana eti na wachezaji wenyewe wanataka kupumzika. Hapana.
Maamuzi ya Simba kukusanya wachezaji iliowakusanya hayakuwa sahihi sana. Ni kwa sababu tu meza ilikuwepo katika mifuko yao ya rambo huku lengo la kwanza likiwa ni kuhakikisha wachezaji hawa hawaendi katika klabu nyingine kubwa kama Yanga na Azam FC.
Simba ilikuwa na malengo mawili. kwanza kuimarisha timu yake, pili ni kuwakomoa wapinzani wao. Inatokea sana. Hata Yanga nayo ilikuwa na tabia hizi hizi wakati ilipozikamata noti. Ilitembeza ubabe ambo wakati mwingine ulikuwa unaathiri wachezaji. Kumbuka jinsi Paul Nonga alivyonunuliwa akitumbukizwa katika kundi la kina Donald Ngoma, Amiss Tambwe na Obrey Chirwa.
Nafasi zinazobakia baada ya klabu kuwa na mastaa ni zile za wachezaji chipukizi ambao wanaendelezwa na kukomaa taratibu. Hakuna mchezaji aliyekamilika ambaye atakubali kukaa benchi kwa kisingizio atacheza baadaye.
Hawa kina Kaheza na Rashid tayari walishakuwa katika kiwango bora ndani ya ligi na kwa lugha fupi walikuwa wachezaji wakubwa katika ligi ambao hawawezi kukaa kwingine wakisubiri nafasi zao kwa wachezaji wenzao ambao wamekomaa kama wao.
Mwisho wa siku watatolewa kwa mkopo. Hata hivyo, hauwezi kuwalaumu kwa sababu mbili. Kwanza kabisa, unaachaje noti zile za Simba? Utazipata wapi tena kama Yanga haina pesa na Azam imefunga usajili wake?
Tuna tatizo, kuna klabu tatu tu katika ligi ambazo zinaweza kukupa pesa inayoeleweka. Kama moja ikiteleza, kama ilivyotokea kwa Yanga, basi wachezaji hawana muda wa kutafakari pindi wanapofuatwa na timu ambayo wanajua kabisa inaweza kuwanyima nafasi ya kucheza. Hiki ndicho kilichotokea kwa Kaheza na Rashid.
Mwisho wa siku na wao wanabakia kuwa wanadamu. Nani hataki pesa? Unachukua pesa, unakaa benchi, unatolewa kwa mkopo kwingineko. Ndio maisha ya kisasa yanavyoenda duniani kwa sasa. Baadaye unaachwa jumla, unakwenda timu ndogo, unapiga soka kubwa halafu unarudi katika timu nyingine kubwa. Kama Hassan Dilunga vile.