Simba, Azam zapelekwa Pemba fainali Shirikisho
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa leo Juni 24, 2026 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo, imesema mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni.
MECHI ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Simba dhidi ya Azam, imepangwa kuchezwa Julai 4, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
Taarifa iliyotolewa leo Juni 24, 2026 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo, imesema mechi hiyo itaanza saa 11:00 jioni.
"Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba ndiyo utakuwa mwenyeji wa mechi hiyo kati ya timu za Simba na Azam za Dar es Salaam itakayofanyika kuanzia saa 11.00 jioni.
"Fainali hiyo ndiyo itakayohitimisha mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa msimu wa 2025-2026," imebainisha taarifa hiyo.
Timu hizo zimefuzu kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali. Simba iliitoa Coastal Union kwa mabao 4-0, wakati Azam ikiing'oa Yanga ambayo ilikuwa inatetea Kombe hilo kwa mabao 3-2.
Tangu msimu wa 2015-2016 ambapo mashindano hayo yalirejea kwa jina la Azam Sports Federation Cup baada ya kusimama kwa takribani miaka 12 kuanzia 2003 hadi 2015, tayari Azam imecheza fainali nne, ikishinda moja msimu wa 2018-2019 ilipoichapa Lipuli bao 1-0.
Fainali tatu ilizopoteza Azam zote ni dhidi ya Yanga ikianzia msimu wa 2015-2016 ilipofungwa 3-1, kisha 1-0 msimu wa 2022-2023 na 2023-2024 kwa penalti 6-5 ilipoanza kuitwa CRDB Federation Cup.
Kwa upande wa Simba, tangu 2015-2016, imecheza fainali tatu na kushinda zote dhidi ya Mbao msimu wa 2016-2017 kwa mabao 2-1, Namungo (2-1) msimu wa 2019-2020 na Yanga (1-0) msimu wa 2020-2021.