Jeuri ya pesa! Mamelodi yatanguliza mastaa saba kwa Jet binafsi

Muktasari:

  • Mastaa hao ni wale ambao walikuwa kambi ya timu ya taifa hilo, Bafana Bafana na wamewasili jana usiku huku wakiwasubiri wenzao ambao wataungana nao leo jioni kutoka Afrika Kusini.

KUNDI la kwanza la msafara wa Mamelodi Sundowns limewasili nchini ambapo mastaa wake saba wametua kwa ndege maalum aina ya Jet.

Mastaa hao ni wale ambao walikuwa katika kambi ya timu ya taifa hilo, Bafana Bafana na wamewasili jana usiku huku wakiwasubiri wenzao ambao wataungana nao leo jioni kutoka Afrika Kusini.

Mastaa walioshuka jana ni kipa namba moja Ronwen Williams, Grant Kekana, Aubrey Modiba, Teboho Mokoena, Themba Zwane, Terrence Mashego na Thapelo Morena ambao wote walikuwa na timu ya taifa lao ya Bafana Bafana iliyokuwa inacheza mechi ya kirafiki nchini Algeria.

Mamelodi ililazimika kuwakodia ndege maalumu mastaa hao kuwahi mchezo huo baada ya jaribio lao la kuomba wachezaji hao wasijimuishwe katika kikosi cha Bafana Bafana kugomewa na kocha wa timu hiyo, Hugo Broos.

Kundi la mwisho la timu hiyo tajiri litawasili nchini leo saa moja usiku likitokea Afrika Kusini tayari kwa mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Yanga utakaopigwa Jumamosi Machi 30 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Timu hizo zilizowahi kukutana katika mechi za raundi ya pili ya michuano hiyo mwaka 2001 na Wasauzi kushinda kwa jumla ya mabao 6-5 zitarudiana siku ya Aprili 5 mjini Pretoria na mshindi atatinga nusu fainali.

Mamelodi kesho Ijumaa itafanya mazoezi yake ya mwisho ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 5:00 asubuhi tayari kwa mechi hiyo ya mkondo wa kwanza.

Yanga ilifika hatua hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1998 ilipocheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mfumo wa sasa kwa kushika nafasi ya pili Kundi D lililoongozwa na Al Ahly, wakati Mamelodi iliibuka kidedea wa Kundi A mbele ya TP Mazembe ya DR Congo.