Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jenga mwili kwa mazoezi haya

Muktasari:

Maumbo hayo ‘sexiest body’ ndiyo yaliyompa umaarufu mkubwa Ronaldo. Staa huyo amewahi kupata tuzo maarufu ya Jarida la Men’s Health Magazine la Marekani ya Mwanaume Bora wa Mwaka mwenye umbo lenye kujengeka na kuvutia.

VIJANA wa kizazi kipya wanaopenda mazoezi huwa na ndoto za kuwa na umbile kama la nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo hii ni kutokana mwanasoka huyu kuwa na mwili wa kuvutia na uliojengeka vyema kimazoezi.

Vilevile vijana hawa hupendelea zaidi wapate tumbo liligawanyika na kuwa na pingilipingili ‘six pack’ na Ronaldo ni mmoja kati ya watu maarufu wanaotumia muda mwingi kufanya mazoezi ya tumbo.

Kwa ujumla kizazi kipya chenye mihemko ya jana ni kawaida kupenda kuwa na miili ambayo imejenga vizuri kuanzia chini mpaka juu lakini wengi hawajui siri ya kujenga mwili uliojengeka kirahisi.

Mwanaume kuwa na mwili wenye mwonekano mzuri ulio na misuli imara na iliyojengeka ni jambo linalopendwa lakini si kila zoezi linaweza kuujenga mwili wote.

Vijana huwa na hulka ya kupenda kuwa na mwonekano mzuri unaovutia pale wanapovaa mavazi ya kisasa.

Maumbo hayo ‘sexiest body’ ndiyo yaliyompa umaarufu mkubwa Ronaldo. Staa huyo amewahi kupata tuzo maarufu ya Jarida la Men’s Health Magazine la Marekani ya Mwanaume Bora wa Mwaka mwenye umbo lenye kujengeka na kuvutia.

Wapo vijana wengi wanaobeba vyuma vizito kiholela ili kuujenga mwili pasipo kufahamu ni aina gani ya mazoezi yanayoweza kujenga mwili wenye mvuto.

Yapo mazoezi yanayokubalika na wataalamu wa tiba za michezo na mazoezi ya viungo kuwa ndio yanakufanya kujenga mwili wote kutokana na uwezo wa kushughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi haya endapo mwanadamu atayafanya mara kwa mara humfanya kuwa na mwili imara na uliojijenga vizuri.

Leo nitawapa mazoezi bora ambayo vijana wakiyafanya kwa umakini huweza kutengeneza mwili uliojengeka kirahisi pasipo kwenda gym wala kutumia virutubisho vya kutunisha misuli.

Zoezi linaloshika namba moja kwa kujenga mwili huwa ni kuogelea, zoezi hili linaujenga mwili kwani linahusisha misuli mingi zaidi kuanzia miguu, kiwiliwili, mikono na kichwa.

Jaribu kuwatazama wavuvi, wapiga mbizi, wanamichezo waogeleaji utagundua wamejengea mwili mzima.

Zoezi la pili ambalo linashika nafasi ya pili kwa kujenga mwili huwa ni kucheza muziki, lakini sio muziki laini kama ilivyo bluzi au taarabu asilia.

Muziki kama wa dansi, Afro, House, Hot Funky, Pop na ngoma za utamaduni zinahusisha kuchezesha misuli mingi mwilini, hivyo kumfanya mchezaji kuwa na misuli imara.

Miaka ya nyuma mwanamziki wa zamani wa Rap, Mc Hammer alikuwa akipungua kilo mbili kila baada ya kutoka katika tamasha alililotumbuiza hii ni kutokana na mwili wake kutumia misuli mwingi wakati wa kucheza mitindo yake.

Zoezi linaloshika namba tatu huwa ni kukimbia, mwanadamu anapokimbia huweza kuhusisha misuli ya mwili mzima. Ukiwatizama wanariadha wengi duniani wana miili imara yenye misuli iliyojijenga vema.

Upo ushahidi wa kitafiti unaonyesha ufanyaji wa zoezi hili huchangia mamilioni ya wakimbiaji kuwa na miili iliyojengeka huku wakiishi maisha marefu zaidi.

Michezo kama sarakasi, michezo ya karate, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mchezo wa rugby yenyewe ndio inashika namba nne kwa kujenga misuli na kumfanya mwanadamu kuwa imara kimwili na kiafya.

Zoezi namba tano huwa ni kutembea nako ni mojawapo ya zoezi ambalo linahusisha misuli mingi ya mwilini, kutembea umbali mrefu ndiko haswa kunakojenga mwili.

Mtindo huu ndio unaowafaa watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kujenga miili yenye afya njema.

Utahitajika kutembea umbali wa wastani angalau kilometa mbili kwa siku katika siku tano za wiki huku ukitembea na kutupa mwili na mikono ili kuishughulisha misuli mingi ya mwili.

Mazoezi ndio chanzo cha kuwa na mwili imara wenye afya njema, hivyo kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ikiwamo kisukari cha aina ya pili, maradhi ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Hii ndiyo sababu inayochangia mamilioni ya wanamichezo duniani pamoja na wafanya mazoezi mepesi ya mara kwa mara kuishi kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na wasiofanya mazoezi.

Lakini swali la msingi zaidi je, mazoezi haya yafanyike kwa muda gani ili kupata matokeo chanya? Kwa kifupi inashauriwa kufanya mazoezi haya kwa siku dakika 30-60 katika siku 5 za wiki.

Vilevile inashauriwa kufuata mwenendo na mitindo bora wa kimaisha ikiwamo mlo kamili uliozingatia kanuni za lishe.

Mwenendo na mitindo mibaya ya kimaisha inayoweza kuchangia kutoweza kujenga mwili hata kama unafanya mazoezi haya ni pamoja ulaji holela wa vyakula vyenye mafuta mengi, wanga na sukari nyingi, unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji tumbaku.

Vyakula ambavyo hupatikana zaidi mitaani, katika migahawa ya kisasa hasa ya Kimagharibi, vyakula vya kusindika hasa vile vinavyuouzwa katika maduka makubwa (supermarkets) pia huchangia kunenepa na kuwa na uzito uliokithiri, hivyo kuharibu ule mwonekano wa ukakamavu wa mwili kutokana na mrundikano wa mafuta mengi.

Kama unapenda kuwa na mwili uliojengeka zingatia mojawapo ya mazoezi haya au fika katika vituo vya mazoezi kwa ushauri zaidi.

Jipangie ratiba ya kufanya mazoezi haya mara kwa na kuwa sehemu ya maisha yako kwani si tu yanaujenga mwili kimazoezi bali pia kukufanya kuwa na afya njema. Fika katika vituo vyenye wataalamu wa lishe na mazoezi kwa ajili ya ushauri zaidi.