Ishu ya Asante Kwasi na Simba iko hivi

Muktasari:

Bado Simba hawana sababu ya kuwa na hofu, wanaweza kutoa hoja zao za msingi kwa CAS na kuomba hukumu, kisha wakalipa na kukwepa adhabu hiyo.

MASHABIKI wa Simba hawana raha tangu usiku wa juzi hii ni baada ya kuwepo kwa taarifa ya chama lao kufungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kufanya usajili kwenye dirisha lijalo kwa kushindwa kumlipa fedha zake, aliyekuwa nyota wao Mghana Kwasi Asante.

Hata hivyo, mashabiki hao hawana sababu ya kuwa na presha kwani, ishu yenyewe ipo simpo tu iwapo tu kama mabosi wa klabu hiyo wataamua kuchangamka sasa kuweka mambo sawa, kwa vile bado wana nafasi ya kupindua meza kibabe kulingana na kanuni na sheria zilizopo.

Simba inadaiwa ilishindwa kumpa mchezaji huyo iliyemsajili mwaka 2017 kutoka Lipuli na kumtema Agosti mwaka juzi na Mghana huyo anayekipiga kwa sasa klabu ya Hafia ya Guinea alikimbilia FIFA kuishtaki klabu hiyo na hukumu ilitoka Februari 24 ikifungiwa kusajili.

Awali, inadaiwa Simba ilishinda kesi ya kwanza dhidi ya Kwasi, kabla ya beki huyo kukata rufaa Mahakama ya Usuluhisi ya Kimataifa ya Michezo (CAS) iliyoamuru alipwe Dola 4,248 ambazo ni sawa na Sh 10 milioni tu ndani ya wiki mbili kuanzia Januari 15, 2020 lakini mabosi wa Msimbazi inadaiwa walishindwa kutekeleza.

Ndipo Februari 26 CAS ikaamua kutoa hukumu hiyo ya kuizuia Simba kusajili kwa dirisha lijalo kwa wachezaji wa kimataifa na wa ndani na kuwatia ubaridi mashabiki wa Simba, hasa ikizingatiwa kuwa chama lao kwa sasa lipo moto kwenye anga za kimataifa na hukumu hiyo huenda ikaiathiri kwenye mipango yao kwa msimu ujao.

Hata hivyo, licha ya kwamba viongozi wa Simba wamekuwa ‘bubu’ kulizungumzia jambo hilo, huku Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez akishindwa kupokea kabisa simu licha ya kutafutwa kutwa nzima ya jana, lakini wanasheria na wadau wa soka nchini wamezungumzia sakata hilo na kudai ni jepesi, hivyo wanasimba wala hawana sababu ya kupaniki.

Mwanasheria Mwita Waisaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema kama suala hilo ni la kweli, Simba bado ina nafasi ya kuomba kupewa hukumu hiyo ili waipitie na hapo wanaweza kupata muda wa kulipa fedha hizo na adhabu kufutika.

“Ni kweli CAS ikihukumu ni nadra kuwepo na nafasi ya kukata rufaa, lakini bado Simba hawana sababu ya kuwa na hofu, wanaweza kutoa hoja zao za msingi kwa CAS na kuomba hukumu hiyo, pengine kutaka kujua pia nani waliyekuwa wanawasiliana naye wakati wa mwenendo wa kesi,” alisema Mwaisaka na kuongeza; “Hapo wanaweza kupata nafasi ya kukwepa adhabu hiyo na pengine kulipa hizo fedha walizotakiwa kuzilipa.”

Naye mchambuzi maarufu wa soka nchini, Shafii Dauda alisema kama ni kweli Simba imeadhibiwa, inaweza kuathirika katika kuimarisha kikosi chao, lakini bado wana nafasi ya kukata rufaa na kuepuka adhabu kwani sio mara ya kwanza hukumu za namna hiyo zinatoka na timu kunusurika.

“Kwa athari ni kweli Simba itashindwa kujiimarisha kwenye nafasi zenye uhitaji wa wachezaji wapya, kwani hukumu ya namna hiyo inazuia timu kusajili mchezaji kutoka kwingine, lakini kwa wale waliopo kikosini na mikataba yao inaisha wanaweza kuwaongeza labda kama watataka kuondoka,” alisema Dauda na kuongeza; “Ila bado wanayo nafasi ya kupindua meza kwani sio mara ya kwanza kwa hukumu za namna hii kutolewa na klabu kuepuka.”

Kwa upande wa Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage alisema ni kweli hata yeye anaijua kesi hiyo ya Kwasi na Simba, lakini anashindwa kuchangia kwa vile anapata shaka ya nyaraka zinazozungumzia hukumu ya kesi hiyo.

“Muhimu ni Simba iwe makini na hizi hukumu zilizoanza kusambazwa tangu juzi usiku, wajiridhishe kwamba ni za kweli, kwa vile dunia ya sasa imebadilika na mbaya zaidi wahusika ni watu wanaotoka Afrika Maghariki wanaosifika kwa umagumashi mitandaoni,” alisema Rage.

Rage alisema kuna maswali mengi yanajengeka kutokana na hukumu hiyo, ikiwamo juu ya uzembe ambao umefanywa na klabu hiyo katika kushughulikia kesi ya Kwasi ambayo ilifahamika kitambo.

“Nahisi kuna uzembe, lakini sitaki kusema sana kwa vile nyaraka zilizopo kwa sasa mtandaoni zinatia shaka, kwani jiulize kama alikuwa akidai dola 11,000 vipi ihukumiwe alipwe dola 4,248.”


WASIKIE SIMBA, TFF

Licha ya kuenea kwa taarifa hiyo ya kesi ya Kwasi, vigogo wa Simba na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamekuwa wagumu kufunguka moja kwa moja kwa kudai hawana taarifa rasmi zaidi ya kuona mtandaoni tu.

Viongozi wa Simba na TFF wamekuwa wagumu kuzungumzia ishu hiyo iliyoleta taharuki kwa mashabiki wa Msimbazi, kwani Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliiambia Mwanaspoti kama viongozi hawana taarifa yoyote rasmi kutoka FIFA wala TFF.

“Hizi kwetu ni propaganda tu hizo, sisi Simba hatujawahi kupata barua ya aina yoyote kutoka FIFA au TFF na ikitokea tutajibu na kama tunadaiwa hatuwezi kukaidi,” alisema Try Again, huku Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Mulamu Nghambi alisema, hizo habari ni za uvumi tu kwa kuwa wao kama uongozi hawajapata taarifa hizo hata siku moja.

“Hata la Kichuya lilikuja hivi hivi, ooh! Simba inafungiwa, imeishia wapi sasa mpaka wamekuja na lingine la Kwasi la miaka mitatu iliyopita. Nakumbuka Kwasi alikuwa anadai huko nyuma ndio, lakini sidhani Kama hajalipwa na wakati huo CEO alikuwa Crescentius Magori akaja Senzo Mazingisa na sasa Barbara Gonzalez ila tungeishapata barua rasmi kama klabu,” alisema.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alipoulizwa kuhusu sakata hilo alijibu; “Taarifa hizo mmezipata wapi sisi kama klabu hatuna, hata hao FIFA hawawezi kufanya kazi kienyeji namna hiyo, sasa ni bora muwaulize FIFA,“ alisema Mangungu.

Hata hivyo, kwa upande wa TFF kupitia kwa Msaidizi wa Katibu Mkuu, Mohamed Mkangara alisema: “Suala hilo liko nje ya uwezo wangu, hata kama lipo au halipo sina mamlaka ya kulizungumzia.”

Katibu Mkuu, Wilfred Kidao naye alipoulizwa alisema; ‘’Niko kikaoni kwa sasa nitakutafuta baadaye.”

Naye Mwanasheria wa TFF Kidifu alisema; “Siwezi kusema hili suala liko mezani kwangu au lah! Ni jukumu la Ofisa Habari kulielezea japokuwa najua taarifa zozote kutoka CAF au FIFA lazima zipite kwetu ndio tuwajulishe klabu.”


MASWALI TATA

Sakata hilo limeibua maswali matano ambayo huenda yanawachanganya mashabiki wa Simba na wadau wengine wa soka nchini ikiwamo;

1.Athari gani Simba itapata kutokana na adhabu hiyo?

Kwa kufungiwa mwaka mmoja kusajili, maana yake Simba italazimika kutumia wachezaji walewale ilionao kikosini pasipo kuleta wapya kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa wale waliopo.

Wasiwasi mkubwa ni uwepo wa kundi kubwa la wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni waliopo kikosini na waliotolewa kwa mkopo hivyo kama wakiamua kuondoka, timu hiyo inaweza kubaki na kundi dogo la wachezaji na kulazimika kutumia wale wa kikosi cha vijana ambao wengi wao bado hawajawa bora na hawajapevuka kiasi cha kutosha kuweza kutimiza mahitaji ya kikosi cha wakubwa. Au iwarudishe walio kwa mkopo au iwaongeze mikataba wachezaji ambao pengine ilikuwa haina mpango wa kuendelea nao. Itakuwa vigumu pia kuwauza wachezaji hata ikija ofa nono kwa kuhofia kukosa wa kuziba mapengo yao.


2. Simba imeshindwaje deni hilo?

Kiujumla kiasi cha fedha kilichosababisha Simba ikutane na rungu hilo ni kiasi kidogo kulinganisha na uwezo wa klabu hiyo kwa sasa.

Kwa hadhi ya klabu ya Simba ilivyo hivi sasa, ni jambo kushangaza kuona wakishindwa kulipa kiasi kama hicho cha fedha ukizingatia wameingiza zaidi ya Sh 1.2 bilioni baada ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ila hata kiwango cha bonasi ambacho imekuwa ikitoa kwa wachezaji wake katika mechi za kimataifa kinafikia pengine hata mara 10 ya fedha hiyo wanayodaiwa na Kwasi.


3. Nani alaumiwe?

Kiutaratibu, taarifa na maagizo kama hayo, FIFA huyatoa kwenda kwa wanachama wake ambapo hapa nchini ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambalo nalo huyafikisha kwa mwanachama wake ambaye ni Simba.

Katika hali hii wengi wanajiuliza ni je Simba walifikishiwa taarifa ndani ya muda sahihi na waliopaswa kufanya hivyo ambao ni TFF au walizipokea taarifa lakini wakazipuuzia?


4. Weledi wa Simba ni wa makaratasi?

Kwa miaka ya hivi karibuni, Simba imejinasibisha kama timu inayoongozwa kwa weledi na kwa mfumo wa kisasa tofauti na klabu nyingine hapa nchini.

Kitendo cha kukumbana na rungu kama hilo kwa kosa la kutolipa stahiki za mchezaji waliyemuacha wakati huohuo kocha wao wa zamani, Sven Vandenbroeck akitangaza kuipeleka klabu hiyo FIFA kwa ajili ya kushinikiza alipwe stahiki zake, kinaacha shaka juu ya ule weledi ambao Simba wanahubiri kila uchao.


5. Mwisho wa haya ni lini?

Inaonekana kama umeshakuwa utamaduni kwa klabu za Tanzania kuachana na wachezaji pamoja na makocha kiholela bila kuwalipa stahiki zao ambazo zina uhalali kwenye mikataba yao na timu.

Hiki kilichotokea kwa Kwasi ni muendelezo wa muda mrefu wa timu zetu katika suala hilo ambalo mwisho wa siku huishia kuziaibisha na kuzifanya ziingie gharama kubwa zisizo na sababu katika kuwalipa watu baada ya kupewa adhabu.

Iliwahi kutokea kwa kina Joseph Shikokoti, Donald Musoti, Joseph Owino, Obrey Chirwa, Patrick Sibomana, Amissi Tambwe na wengine wengi, hii ya Kwasi ni muendelezo tu.


WASIKIE WADU

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, alisema tatizo kubwa ni uhuni wa viongozi wengi wa klabu hizo kubwa.

“Viongozi wa mpira hawabadiliki, wapo vile vile miaka nenda rudi, wanashindwa kuendana na wakati uliopo hivyo lazima wajue kuwa wanazigharimu hizi timu.

“Mchezaji au kocha kama humtaki, mlipe chake akatafute maisha sehemu nyingine, lakini sio unamuacha tu na unajua anadai, ndio haya sasa yanayotokea. Tatizo ni kwamba hizi klabu kubwa viongozi huwa wanagawanyika, kuna baadhi utakuwa wanataka mchezaji aondoke, wengine abaki, sasa hapo mwisho wakifikia uamuzi ndio wanamuacha bila kumlipa stahiki zake.

“Hii adhabu ni mbaya kwa Simba kwani watabaki na wachezaji wale wale na unajua kuwa wanashiriki mashindano ya kimataifa hivyo itapunguza hata ushindani kwani waliopo watakuwa huru kwa sababu wanajua hakutakuwa na wachezaji wengine wapya wa kuwapa changamoto.

“Hili liwe fundisho kwao na kwa klabu nyingine. Viongozi wabadilike wajue tuko katika dunia ya utandawazi. Wafanye uamuzi wa maana ili yasije tokea tena kama haya,” alisema Mmachinga.

Naye mchambuzi wa soka, George Ambangile alisema kulingana na kikosi cha Simba cha sasa kilivyo jambo hilo linaweza lisionekane kuwaathiri moja kwa moja licha ya kwamba hawawezi kukwepa athari.

“Ukweli ni kwamba kila msimu unapomalizika timu zote duniani zinapenda kuboresha vikosi vyao kwa kusajili wachezaji wapya wenye ubora mkubwa ili kuongeza ufanisi.

“Sasa timu isiposajili inawafanya wachezaji waliopo kikosini kubweteka kwa sababu wanakuwa na uhakika wa namba na wanakuwa hawana washindani wa kweli katika nafasi zao. Hivyo hata Simba inaweza kuwaathiri zaidi hasa kwa michuano ya kimataifa,” alisema Ambangile.