Ilikuwa lazima Xavi aitose Barcelona

Muktasari:
Wengi wanaamini Xavi ameamua kubaki Uarabuni kwa sababu ya pesa, lakini kiuhalisia kuna sababu nyingine za msingi sana ambazo zimemfanya aikatae kazi ya ndoto yake.
BARCELONA,HISPANIA .INAWEZEKANA ulikuwa uamuzi mgumu sana kuuchukua, lakini, Xavi Hernandez alikuwa na sababu zake za msingi zilizomfanya aitose Barcelona.
Wengi waliamini Xavi anarudi Barcelona baada ya mabosi wa klabu hiyo Oscar Grau na Eric Abidal kumfuata Qatar wakiwa na ofa mkononi ya kumtaka arudi kwenye klabu yake ya utotoni.
Lakini, kwa mshangao wa wengi Xavi aliikataa ofa hiyo na kuamua kubaki zake Al Sadd na kuifanya Barcelona kumchukua Quique Setien kutoka Real Betis kuja kurithi mikoba ya Ernesto Valverde, aliyetimuliwa.
Wengi wanaamini Xavi ameamua kubaki Uarabuni kwa sababu ya pesa, lakini kiuhalisia kuna sababu nyingine za msingi sana ambazo zimemfanya aikatae kazi ya ndoto yake.
Kama ipo ipo tu
Hii ndiyo sababu kubwa ya Xavi kugoma kurudi Barcelona, Japokuwa Setien amepewa mkataba wa hadi Juni 2022, lakini wakati Xavi anakataa kazi hiyo aliamini kuwa bado ana nafasi ya kuja kuwa kocha wa Barca katika siku za usoni, hata kama itachukua muda mrefu.
Hivyo akaona kuliko kuichukua timu yenye majanga katikati ya msimu ni bora asubiri miaka ijayo wakati atakapopewa timu mwanzo wa msimu na kuanza nayo maana alijua ikitokea akapewa timu wakati huu na ikachemka basi atajiharibia yeye kama kocha kijana ambaye baada ya kucheza soka kwa mafanikio makubwa sasa sasa hivi anapambana kutengeneza jina lake kama kocha, ndiyo maana ameamua kusubiri apewe timu katika kipindi ambacho anaweza kuanza nayo msimu.
Heshima kwa Ernesto Valverde
Xavi ni mtu wa soka na anamuheshimu sana aliyekuwa kocha wa Barcelona. Hivyo hakutaka kuchukua mikoba ya kuinoa Barca kwa staili ile, aliamini mchakato mzima wa kumpa timu ulimkosea heshima Valverde ndiyo maana aligoma na kuona kama mtu wa soka haikuwa sahihi. Kitendo cha kumfuata yeye wakati Valverde akiwa bado kocha wa Barcelona hakukipenda na aliona si jambo la busara kwa yeye kama kocha kijana kuchukua timu kutoka kwa Valverde kwa staili ile.
Analipa fadhila kwa Al Sadd
Miamba hiyo ya Qatar ilimpa Xavi nafasi ya kuanza maisha yake ya ukocha baada ya kustaafu soka na ndiyo maana hakutaka kuharibu uhusiano wake na timu hiyo iliyomfungulia milango katika tasnia ya ukufunzi. Mkataba wake wa sasa na Al Sadd unaisha Juni 2021 na mpango wa awali ulikuwa afundishe hadi mwisho wa mkataba wake kisha achukue mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya Qatar itakayokuwa inajiandaa na Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini humo.
Usaliti kwa wachezaji wake
Xavi aliona kukubali ofa ya kuinoa Barcelona ni kuwasaliti wachezaji wake hasa katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inakabiliwa na mechi ya fainali ya Kombe la Qatar Ijumaa hii dhidi ya Al Duhail.
Hivyo aliona kuondoka kabla ya fainali hiyo ni kuwasaliti wachezaji wake waliompigania hadi kufika fainali. Pia fainali hiyo inamfanya awe na nafasi ya kubeba taji la pili kama kocha baada ya kiangazi mwaka jana kutwaa taji la Super Cup ya Qatar.
Siasa za Barcelona
Inaambiwa siasa za klabu ya Barcelona nazo ni sababu kubwa kwa Xavi kukataa nafasi ya kurudi Barcelona. Iko hivi Xavi anamsapoti Victor Font anayetaka kugombea urais wa Barca kwenye Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo mwaka 2021, hivyo kama angekubali kurudi Camp Nou wakati huu timu ikiwa chini ya Rais Josep Bartomeu, inamaana angeshindwa kuendelea kutoa sapoti kwa Font kwenye uchaguzi na kwa akili ya kawaida angeonekana anamsapotu Bartomeu na hiyo ingemfarakanisha na rafiki yake Font.
Hata wakati anawatosa Grau na Abidal walipompa ofa ya kurudi Camp Nou alijua fika kuwa hata akiikataa atapata nafasi ya kufundisha Barca siku rafiki yake Font akishinda uchaguzi wa mwaka 2021.
Bartomeu ni tatizo
Rais wa sasa wa Barcelona ana matatizo yake na inaonekana hapatani na magwiji kibao kwa klabu hiyo ndiyo maana si Xavi pekee ambaye amegoma kurudi Barca baada ya kupata nafasi hiyo, wapo wengi tu.
Mbali na Xavi kocha wa timu ya Taifa ya Uholanzi, Ronald Koeman, naye amegoma kurudi kufundisha Barcelona. Carles Puyol naye aliwahi kutataa ofa ya Bartomeu, kurudi Barca kwenda kuwa Mkurugenzi wa Soka, Victor Valdes aliwahi kukubali kurudi Barca, lakini alitimuliwa baada ya kugombana na Patrick Kluivert. Jordi Cruyff naye anakaribia kuchukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya Ecuador, licha ya kuwa na ofa kutoka Barcelona.
Hii yote ni uthibitisho Bartomeu ndiyo maana mbali na Xavi magwiji kibao wamegoma kurudi katika klabu hiyo na wengi wanaonekana kusubiri hadi uchaguzi wa mwaka 2021 upite na kama akitolewa ndiyo warudi katika klabu yao pendwa.