Ihefu yaiwahi Simba mapema

Muktasari:

  • Simba na Ihefu zinatarajia kukutana mara mbili Aprili zikianza na mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa Aprili 7, Dar es Salaam na siku chache kuvaana Ligi Kuu Bara jijini Mbeya

BAADA ya kukusanya pointi sita kwa vigogo Yanga na Azam FC, Kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila amerudisha timu haraka kambini tayari kujifua kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Aprili 7 huku akikiri kuwa na dakika 180 ngumu.

Simba na Ihefu zinatarajia kukutana mara mbili Aprili zikianza na mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaopigwa Aprili 7, Dar es Salaam na siku chache kuvaana Ligi Kuu Bara jijini Mbeya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila alisema walitoa mapumziko kwa timu na sasa wamerudi kambini na wanaanza kujifua tayari kwa ajili ya michezo hiyo miwili ndani ya mwezi mmoja ambayo yote amekiri kuwa ni muhimu kwao.

“Tuna dakika 180 ngumu tunahitaji kujiandaa mapema kwa kujiweka fiti kutokana na kukutana na wapinzani ambao wamepata wakati mzuri wa kucheza mechi nyingi mfululizo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wanayoshiriki na sisi tulikuwa na mapumziko kupisha mechi mbili za timu ya taifa.

“Kwa asilimia kubwa kikosi kipo ni wachezaji wachache walioitwa timu za taifa hivyo tutaendelea kujiweka fiti ili muda ukifika timu inakuwa bora ikiwa ni pamoja na wachezaji kuandaliwa kisaikolojia kuhakikisha wanatumia kila nafasi watakayotengeneza ili kuweza kujiweka nafasi nzuri,” alisema.

Katwila alisema kikosi kimeimarika baada ya wachezaji kuingia kwenye mfumo na wameanza kuona utofauti na malengo yao yanaenda kutimia kutoka kuwa kwenye presha ya kushuka daraja na sasa kuwania tano bora kwenye msimamo.

Alisema ubora uliopo kwenye kikosi chao hawataki kuona unaanza kupotea kutokana na kutokukaa pamoja kwa muda mrefu ndio maana wamewarudisha wachezaji haraka kambini ili kuendelea kuwaweka kwenye hali ya ushindani.