Ihefu mpya bila Simkoko

Muktasari:

  • Ihefu ilianza msimu uliopita chini ya Zubery Katwila kama kocha mkuu kabla ya baadaye kutua kwa Juma Mwambusi ambaye hakudumu muda mrefu kwani aliondoka bila sababu kuwekwa wazi, kisha jahazi kupewa Simkoko aliyefukia mashimo na kuifanya timu iwe bora tofauti na ilivyoanza msimu.

TAYARI timu mbalimbali zimeingia kambini kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu kama ilivyo kwa Ihefu iliyomaliza ligi ikiwa nafasi ya sita kwa kuvuna alama 39, huku taarifa zikieleza ndoa ya klabu hiyo na kocha mkongwe wa kimataifa, John Simkoko ikifikia tamati.

Ihefu ilianza msimu uliopita chini ya Zubery Katwila kama kocha mkuu kabla ya baadaye kutua kwa Juma Mwambusi ambaye hakudumu muda mrefu kwani aliondoka bila sababu kuwekwa wazi, kisha jahazi kupewa Simkoko aliyefukia mashimo na kuifanya timu iwe bora tofauti na ilivyoanza msimu.

Ihefu iliyokuwa inaburuza mkia kwa muda mrefu ilimaliza katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 39 kutokana na mechi 30, huku ikiweka rekodi ya kuitibulia Yanga iliyokuwa imecheza mechi 49 bila kupoteza kwa kyuifunga mabao 2-1 katika pambano lililopigwa Novemba mwaka jana jijini Mbeya.

Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza, Simkoko ameshamalizana na mabosi wa timu hiyo kwani mkataba wake ulikuwa wa miezi sita pekee.

Alipotafutwa kocha huyo mwenye historia tamu kwenye soka la Bongo alisema uulizwe uongozi juu ya jambo hilo sababu wao ndio wanaujua ukweli kamili.
Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila kila alipotafutwa hakuweza kutoa ushirikiano juu ya jambo hilo zaidi ya kusema;

"Nitakutafuta baadaye."
Kwa upande wake, Katwila alisema maandalizi ya msimu ujao tayari yameshaanza ikiwa pamoja na kuboresha kikosi chao katika dirisha hili la usajili.

"Hatutakuwa na mabadiliko makubwa sababu dirisha dogo la Januari tulifanya usajili wawachezaji wengi na tuliacha wengi hivyo sahivi ni maandalizi ya kawaida.

"Kuhusu nani atatoka na nani ataingia nadhani muda ukifika wahusika wataweka wazi ila lazima mabadiliko yafanyike," alisema Katwila.

Ihefu ndio timu ya kwanza kupanda Ligi Kuu kupitia mfumo wa hatua ya mtoano ilipofanya hivyo msimu wa mwaka 2020/21 kwa kuiondoa Mbao.