Ibrahimovic aliamsha, arusha kijembe

Muktasari:

Awali, Vela alianza kuifungia Los Angeles mabao mawili kabla ya Ibra Cadabra hajasawazisha kwa shuti kali la mguu wa kushoto, kisha akapiga jingine la mguu wa kulia na kumalizia na lile la kichwa ambayo yaliamsha msisimko katika mchezo huo.

Kama ulidhani amekwisha, basi sahau! Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na Barcelona, Zlatan Ibrahimovic amepiga 'hat trick' akiifungia klabu yake ya LA Galaxy dhidi ya Los Angeles FC katika mechi ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), juzi.
Nyota huyo mwenye asili ya Sweden alifunga mabao hayo katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Los Angeles, kisha akarusha kijembe kwa wapinzani akiwaita kuwa 'vijana' wasio na ubavu wa kumtikisa.
Ibrahimovic pia alimkejeli mshambuliaji tegemeo wa Los Angeles, Carlos Vela, ambaye anaongoza katika msimamo wa ufungaji mabao mengi katika ligi hiyo akiwa nayo 21 msimu huu, lakini akamuita kuwa ni "kijana" akimfananisha na magari ya mashindano ya langalanga ya Ferrari ilhali yeye ni gari kubwa aina ya Fiat.
Awali, Vela alianza kuifungia Los Angeles mabao mawili kabla ya Ibra Cadabra hajasawazisha kwa shuti kali la mguu wa kushoto, kisha akapiga jingine la mguu wa kulia na kumalizia na lile la kichwa ambayo yaliamsha msisimko katika mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo kumalizika, mchezaji huyo alikaririwa akisema, "ukisema wewe ni Ferrari kwenye ligi ni lazima utambue kwamba zipo pia Fiat" akijibu kauli ya Vera aliyewahi kukaririwa akijiita kuwa Ferrari kutokana na kasi yake ya kutupia mabao nyavuni.
Alihoji,"Lakini pia kwa sababu (Vela) yupo katika kilele (cha mafanikio). Je ana umri gani? (miaka) 29. Na anacheza MSL (Ligi Kuu ya Marekani). Nilipokuwa na miaka 29 nilikuwa nakipiga Ulaya, hii ni tofauti kubwa."
Hiyo siyo mara ya kwanza kwa mchezaji aliyewahi pia kukipiga Inter Milan na Ajax, kwani aliwahi pia kuwakejeli wachezaji mbalimbali aliowahi kukabiliana nao katika ligi mbalimbali barani Ulaya. 
Ibrahimovic alisema alipata mzuka zaidi na kuamua kukipigania kikosi chake baada ya kufikiria kwamba wapinzani wao wangetamba zaidi baada ya mchezo kumalizika, ikizingatiwa kwamba timu hizo zina utani wa jadi.
Mchezaji huyo amefunga jumla ya mabao 41 tangu alipojiunga na MLS miaka mitatu iliyopita akiwa amecheza miecho 44 na jumla ya mechi 520 tangu alipoanza kucheza soka.