Ibenge ataka wasaidizi watatu

Muktasari:
- Ibenge ambaye ametoka kuifundisha Al Hilal ya Sudan ametua Azam hivi karibuni, huku akisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye uwezekano wa kuongezeka.
KOCHA mpya wa Azam FC, Florent Ibenge amewapendekeza makocha wasaidizi kutoka Al Hilal aliyokuwa anaifundisha kabla ya kutua klabuni hapo na mabosi Chamazi wamethibitisha hilo.
Ibenge ambaye ametoka kuifundisha Al Hilal ya Sudan ametua Azam hivi karibuni, huku akisaini mkataba wa mwaka mmoja wenye uwezekano wa kuongezeka.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, kocha huyo alivyofika tu akawaambia mabosi hao mahitaji yake ikiwemo suala zima la benchi la ufundi.
"Anataka kuja na kocha msaidizi wake wa makipa na 'video analyist' na amewaambia mabosi wa Azam alikuwa na wakati mzuri na makocha hao akiwaona bora kuliko wengine wote.
"Hata hivyo mmoja kati ya kocha msaidizi ambaye ametakiwa ni Anicet Kiazayidi aliyewahi kuifundisha Tabora United, kwani ni marafiki sana."
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi' alisema kila kocha anayekuja katika timu huwa anakuwa na wasaidizi wake na kuondoka nao.
"Ni kawaida katika soka kwa kocha kuja na wasaidizi wake na kuondoka nao, siyo kwa Ibenge tu, hata aliyeondoka alifanya hivyo kwa hiyo ni kweli," alisema Zakazi na kuongeza;
"Yapo mapendekezo yake aliyokuja nayo na mahitaji yake muhimu kama kocha ni benchi la ufundi ambalo yeye sasa ndio anajua anataka kumuongeza nani wa kufanya naye kazi."
Makocha hao waliwahi kufanya kazi pamoja katika kikosi cha Al Hilal ambako Ibenge alikuwa ndiye mkuu na Anicet akiwa katika benchi la ufundi.
Ikumbukwe kuwa makocha hawa wawili waliichapa Yanga katika michuano tofauti, huku Ibenge akiianza kimataifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2-1 na Anicet aliinyoa katika ligi ya ndani 3-1 na kusababisha Kocha Miguel Gamondi kusitishiwa mkataba baada ya kipigo hicho.
Azam chini ya kocha wake aliyepita Rachid Taoussi ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu ikiwa na alama 63, ikishinda mechi 19 sare sita na kupoteza mitano kati ya michezo 30.