Huyu hapa mshindani wa Msuva Iraq
Muktasari:
- Msuva amesajiliwa na klabu hiyo akitokea Al Najma ya Saudi Arabia alikodumu kwa msimu mmoja na kufunga mabao manne kwenye michezo 15.
WINGA wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Simon Msuva wikiendi iliyopita alitambulishwa na Al Talaba inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq.
Msuva amesajiliwa na klabu hiyo akitokea Al Najma ya Saudi Arabia alikodumu kwa msimu mmoja na kufunga mabao manne kwenye michezo 15.
Licha ya nyota huyo wa zamani wa Yanga kutambulishwa kikosini hapo, lakini Mnigeria Austin Amutu (31) aliyesajiliwa msimu huu akitokea Al Jandal, anaonekana kuwa mpinzani wa Msuva.
Wote wawili rekodi zao zinashabihiana kwa Msuva ambaye alitokea Najma alifunga mabao manne kwenye mechi 15 huku Amutu akifunga bao moja kwenye mechi 12.
Mara ya mwisho kwa kiungo mshambuliaji raia wa Nigeria kufunga mabao mengi ni msimu wa 2019–2022 akiwa na Al Masry ya Misri akiweka kambani mabao 18.
Hata hivyo, mchezaji huyo hajawahi kufunga zaidi ya mabao 18 tangu aanze kucheza soka la kulipwa Nigeria.
Mapema wiki hii Msuva alizungumza na gazeti hili na kusema "Kilichobaki kwa sasa ni mimi tu kuwafanyia kazi yao. Binafsi sina shaka na uwezo wangu, nipo tayari kuonyesha Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye vipaji vingi vya soka. Nina shauku kubwa ya kuanza maisha yangu mapya ya utafutaji Irak, najua ni nchi nzuri kama ilivyo Saudia."
Al Talaba itakuwa timu ya sita kwa Msuva kuichezea nje ya Tanzania, chama lake la kwanza lilikuwa Difaa El Jadida alilojiunga nalo Julai 2017 baada ya kuonyesha makali yake ndani ya miaka mitatu kwenye Ligi ya Morocco, Wydad Casablanca ilijivunia naye na kumsajili lakini hakudumu kwa vigogo hao kutokana na ishu za madai zilizowafanya kufikishana Fifa.
Baadaye Msuva aliibukia Saudi Arabia alikoanza kwa kuichezea Al-Qadsiah na mkataba wake ulipomalizika alirejea Afrika kujiunga na JS Kabylie ya Algeria, lakini mambo hayakumwendea vizuri mkataba wake ulikatishwa na ndipo alipoamua kurejea tena Saudia Arabia na alijiunga na Al-Najma aliyoichezea msimu uliopita.