Huyo Luis Miquissone balaa tupu!

Muktasari:

BAO moja alilofunga dhidi ya AS Vita Club juzi, limemfanya mshambuliaji Luis Miquissone wa Simba kuzidi kuwa tishio katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

BAO moja alilofunga dhidi ya AS Vita Club juzi, limemfanya mshambuliaji Luis Miquissone wa Simba kuzidi kuwa tishio katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Baada ya kuwa gumzo kwa kufunga bao pekee la ushindi la Simba dhidi ya Al Ahly na kutangazwa kuwa mchezaji bora wa wiki, kisha akaja kufunga tena dhidi ya Al Merrikh, bao alilopachika juzi dhidi ya Vita, limemfanya Luis awe kinara wa mabao katika hatua ya makundi akiwazidi ujanja, Ayoub El Kaabi wa Wydad Casablanca na Mohamed Ben Romdhane wa Esperance waliofunga matatu kama yeye.

Luis licha ya kuwa na idadi sawa ya mabao na nyota hao, lakini amewafunika kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao kwani yeye kiujumla amehusika katika kuzalisha mabao mengi ya Simba kuliko wenzake katika timu yake.

Nyota huyo kutoka Msumbiji amehusika katika mabao matano kati ya tisa ya Simba iliyopachika katika hatua ya makundi ikiwa sawa na 55.56% ya mabao yote ya timu yake akiwa amefunga mabao matatu na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao mengine.

Ni tofauti na El Kaabi aliyehusika na mabao manne kati ya saba ya Wydad akifunga matatu na kuasisti moja katika hatua ya makundi ikiwa ni sawa na 57.14% kama ilivyo kwa Romdhani aliyechangia mabao manne kati ya nane ya Esperance.

Akizungumzia mafanikio hayo, Luis alisema mafanikio yake ni juhudi za pamoja za timu.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Naamini hiki kinachotokea ni mchango wa pamoja wa timu nzima, hivyo nawashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki,” alisema Luis aliyesajiliwa kutoka UD Songo ya Msumbiji.

Ukiondoa Luis, wachezaji wengine ambao wameifungia Simba katika hatua ya makundi ya ligi hiyo ni; Clatous Chama na Chris Mugalu ambao kila mmoja amefunga mawili, Mohamed Hussein na Larry Bwalya wakifunga moja.