Huyo Chama kaiva, mbona mtamkoma
Muktasari:
Chama pamoja na kikosi cha Simba walitarajiwa kutua nchini jana Jumatano wakitokea nchini Afrika Kusini walipokuwa kwenye maandalizi yao nje kidogo ya mji wa Rostenburg katika Hoteli ya The Royal Marang.
KAMA hujui ubora wa Mzambia Clatous Chama umeongezeka maradufu na kasi aliyoanza nayo huko Afrika Kusini katika kipindi cha msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano mengine atatisha sana, jambo linalomfanya mwenyewe afichue kilicho nyuma yake.
Achana na mambo ya msimu uliopita kama lile bao lililowavusha Simba hatua ya makundi, lakini katika kipindi cha maandalizi yao huko frika Kusini, Chama anaonyesha kiwango cha juu sambamba na kupiga mabao ya maana. Kati ya mechi nne ambazo wamecheza, Chama amefunga mabao matatu kati ya 10, mawili kwenye ushindi wa 4-1 dhidi ya Platnum Stars na akafunga moja lililowapa sare ya 1-1 na Orlando Pirates.
Kutokana na mambo hayo, Chama ameliambia Mwanaspoti kuwa utamu huo umetokana na mazoezi binafsi anayofanya, lakini pia kampani anayopata kutoka kwa wachezaji wenzake.
“Huo ni utaratibu wangu niliojiwekea, sio kila siku lakini mara kwa mara nimekuwa nafanya mazoezi yangu binafsi kila baada ya kumaliza programu ya mwalimu (Patrick Aussems),”alisema Chama ambaye wakati kikosi hicho kipo kwenye kambi Afrika Kusini, mwandishi wa stori hii alikuwa akimshuhudia akifanya mazoezi hayo.
“Mbali na hilo bidii, kujituma pamoja na kushirikiana na wenzangu kumenifanya nifikie hapa nilipo,”alisema mchezaji huyo ambaye amepachikwa jina la utani Mwamba wa Lusaka.
Kiungo huyo mshambuliaji alisema kutokana na hilo, msimu huu anaona utakuwa mzuri kwake pamoja na timu kutokana na mipango iliyowekwa kwenye klabu.
“Hakuna mtu anayejua mbele yake inakuwaje, lakini ndoto za kila mtu kutokana na anachokifanya ni kutegemea mazuri, tunamwomba Mungu kwa hilo.”
Chama pamoja na kikosi cha Simba walitarajiwa kutua nchini jana Jumatano wakitokea nchini Afrika Kusini walipokuwa kwenye maandalizi yao nje kidogo ya mji wa Rostenburg katika Hoteli ya The Royal Marang.