Mubesh ataja siri ya ubingwa Ureno
Muktasari:
- Timu hiyo ilikuwa Ureno ikishishiriki mashindano ya Iber Cup kwa vijana U-14 chini ya kocha Mubesh ambaye aliwahi kuhudumu kwenye kikosi cha KMC kilichoshika daraja msimu uliotamatika.
BAADA ya kubeba ubingwa wa Iber Cup nchini Ureno, Kocha wa TDS Akademi, Adam Mubesh amesema ushindani walioupata kwenye mashindano hayo umewapa wachezaji nafasi ya kujifunza mitindo mbalimbali ya kiuchezaji.
Timu hiyo ilikuwa Ureno ikishishiriki mashindano ya Iber Cup kwa vijana U-14 chini ya kocha Mubesh ambaye aliwahi kuhudumu kwenye kikosi cha KMC kilichoshika daraja msimu uliotamatika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mubesh alisema mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa kutokana na kushirikisha klabu na akademi zenye viwango vya juu kutoka sehemu mbalimbali duniani.
"Yalikuwa mashindano mazuri yenye ushindani mkubwa, hasa ukizingatia ushiriki wa klabu na akademi za kimataifa. Unapata ladha tofauti za uchezaji kila unapokutana na timu kutoka mataifa mbalimbali," alisema Mubesh.
Aliongeza kuwa, mechi ambayo ilimfanya abadili mbinu ilikuwa dhidi ya New York Soccer Club ya Marekani ambayo alikiri wapinzano hao wanacheza kwa kutumia nguvu nyingi na kasi.
"Kwa upande wa timu kutoka Hispania, walikuwa na ufundi mkubwa na mbinu za hali ya juu. Hivyo kila mchezo ulikuwa darasa jipya kwetu na kwa wachezaji," alisema.
Mubesh alisema lengo kuu la kushiriki michuano hiyo halikuwa kutwaa ubingwa pekee, bali pia kuwapa wachezaji uzoefu wa kucheza katika mazingira ya kimataifa na kuongeza kiwango chao cha kujiamini.
"Kikubwa tulitaka kuwapatia wachezaji uzoefu na kuzoea mazingira magumu hii itawasaidia kujiamini zaidi, kuzoea mazingira tofauti na ya nyumbani na kuwajenga kama wachezaji mmoja mmoja pamoja na timu kwa ujumla," alisema.
TDS ilimaliza mashindano hayo ikiweka rekodi nzuri ikishinda mechi zote sita ilizocheza huku ikiruhusu bao moja mbele ya timu kutoka Marekani, Ureno, Hispania, England na mataifa mengine.