Hukumu ya Beno ndani ya saa 72

Muktasari:

  • Kipa huyo aliyewahi kuichezea Simba na Yanga alidaiwa kuondoka kambini saa chache kabla ya mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, huku Ofisa habari wa klabu hiyo akidai aliondoka bila kuaga kupitia vyombo vya habari.

BAADA ya sakata la kutoroka kambini lililomkumba, Kipa wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya hukumu yake itatolewa ndani ya dakika 72.

Kipa huyo aliyewahi kuichezea Simba na Yanga alidaiwa kuondoka kambini saa chache kabla ya mechi dhidi ya Yanga iliyochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, huku Ofisa habari wa klabu hiyo akidai aliondoka bila kuaga kupitia vyombo vya habari.

Klabu hiyo iliamua kutoa taarifa katika mitandao yake ya Kijamii na kabla ya mechi hiyo, na baadae walitoa wito wa kumtaka afike kwenye kikao cha kamati ya nidhamu lakini mchezaji huyo aligomea wito huo.

Mwanaspoti ilizungumza na Ofisa habari wa klabu hiyo, Hussein Masanza ili kujua kinachoendelea ambapo alisema   kinachosubiriwa ni uamuzi wa kamati unaotarajiwa kutoka wakati wowote.

"Ndani ya saa 72 kuanzia sasa kamati inayoundwa na mwanasheria wa timu na baadhi ya wajumbe itatoa uamuzi na hukumu kuhusu mchezaji wetu, ili suala hili lifahamike kama litafika mwisho au kuendelea hatua nyingine," amesema Masanza.

"Hivyo mashabiki zetu watulie. Kila kitu kitafahamika ili kuondoa hii sintofahamu iliyopo kutokana na wengi kuuliza juu ya uamuzi wa mwisho wa kamati wa hatima ya kosa la Beno."