Hojbjerg asimulia alivyonufaika na mafunzo ya Pep
Muktasari:
- Ilipofika saa tisa na nusu, Pep aliwaaga waachezaji na kundi lake kwa jumla waliokuwa wakiendelea kufurahia, akawaambia usiku mwema kisha akamshika mkono Valentina (mkewe) kama mtoto wake na kwenda zao kulala. Nje mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha
TOLEO lililopita kwenye Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau aliangazia mazingira ya Bayern yalivyokuwa hasa hali ya kukata tamaa ikiwamo uamuzi wa Pep kumpanga mchezaji Hojbjerg aliyeonekana kama hakuwa amekomaa kwa mechi kubwa kama hiyo, lakini mwishowe ushindi ulipatikana na wachezaji wakafanya sherehe. Endelea…
Ilipofika saa tisa na nusu, Pep aliwaaga waachezaji na kundi lake kwa jumla waliokuwa wakiendelea kufurahia, akawaambia usiku mwema kisha akamshika mkono Valentina (mkewe) kama mtoto wake na kwenda zao kulala. Nje mvua ilikuwa ikiendelea kunyesha.
Baada ya hapo, Bayern wakaanza safari ya kwenda kwao Munich wakiwa na kombe lao walilolibeba katika Mji Mkuu wa Berlin baada ya kuilaza Dortmud, mafanikio ambayo yamekuwa na maana kwa Pep katika mwaka huo, maelfu ya mashabiki walikuwa wakiwasubiri katika eneo maarufu la Marienplatz, tayari kwa kufurahia ushindi mwingine wa msimu.
Tukiwa katika safari hiyo, nilifanya mazungumzo na Hojbjerg (Pierre) pamoja na Lahm. Nilimuuliza Hojbjerg kuhusu alichojifunza kutoka kwa Pep. “Kuwa makini na jasiri zaidi na mpira, alinionyesha umuhimu wa kucheza bila ya hofu, yaani kucheza tu soka lako bila kujali kama unakabiliana na Xabi Alonso au mchezaji ambaye bado mchanga.
“Kucheza kwa ujasiri bila woga na kuonyesha uwezo wako, ni kama Pep mwenyewe anavyosema,
“Unapokuwa bado mchanga unakuwa na hofu au mwenye kusitasita katika baadhi ya mambo lakini hilo haliwezi kukufikisha popote, unatakiwa kujitoa kwa kila kitu kama unataka kuongeza ubora wako siku hadi.
“Pep alinisisitizia nisiache hofu ikanikaa, au nisiwe mwenye kusitasita ninapocheza, pia amenifunza mengi kuhusu mbinu za uchezaji ikiwamo ukabaji, nimejifunza kutulia kutokuwa na haraka ya kupanda wakati ambao wachezaji wenzangu wamepanda wanashambulia, ni hivyo hivyo inapofika wakati wangu wa kupeleka mashambulizi.
“Amenifundisha kila kitu kuhusu mbinu sahihi na amenifunza namna ya kucheza kwa utulivu, umakini na ujasiri, nilikuwa na wakati mgumu msimu huu na hakika Pep amenisaidia, aliniambia ninachohitaji kufanya ni kujituma katika dakika 90 za siku ya soka, hizo dakika 90 lazima wakati wote niwe mpambanaji. Akaniambia kama nitafanya hivyo woga utanitoka kuhusu mchezo.”
Hojbjerg alijiunga na Bayern mwaka 2012 wakati akiwa ndio kwanza ana miaka 16 na akawa mwenye kuhaha na ratiba ya mazoezi ya siku nne kwa wiki.
“Ukweli, nilikuwa mdogo na mwili wangu haukuweza kukabiliana na kazi nyingi, kimsingi nilikuwa mwenye machungu karibu kwa kipindi chote cha mwaka na mwaka huu nikiwa na Pep hali imekuwa hivyo hivyo, kuna wakati nilikuwa na tatizo la kuwa katika mstari mmoja na wachezaji wakubwa na wakongwe katika mazoezi ya siku sita kwa wiki.
Perarnau: Kwa hiyo kwako msimu umekuwa zaidi katika kujifunza na si kushindana uwanjani.
H (Hojbjerg): Ni kweli ninapotoka tu kitandani asubuhi wakati wote nilikuwa nikijiambia,
“Leo itaweza kuwa bora kuliko jana, leo nitakuwa mchezaji mzuri, nitajifunza kitu kipya, napenda kujifunza kitu kipya kila siku na nataka niendelee kuwa bora siku hadi siku.
“Nafikiri Pep ameona kila kitu kwangu na najaribu kuchukua kila kitu anachonifundisha na kuvitumia katika soka langu, nataka kufuata kile moyo unachonituma ma kujaribu kufanya mambo ambayo yatanisaidia kupiga hatua.
“Mimi si mtu mwenye kuvimba kichwa, bali ni mwenye kujiamini na kuna wakati naharakisha katika kuja na hitimisho au jibu uamuzi wangu ndio bora zaidi, nimelazimika kujifunza watu wengine nao kuna wakati wanakuwa na majibu na maamuzi mazuri na kwa Pep hakika hilo limejidhihirisha.
“Amekuwa akinionyesha suluhisho lililo bora zaidi, kwa mfano hii ni mara ya kwanza nimeelewa unahitaji kuwa juu katika mbinu zote za eneo la ulinzi pamoja na kuwa na nidhamu ya juu hasa pale unapotaka kucheza katika soka la hadhi ya juu.
“Kwa sasa naelewa ni vipi kuna umuhimu wa kuwa makini na mwenye fikra sahihi ili kuimarisha safu ya ulinzi, kuwa makini kila wakati inapotokea mchezaji wa timu pinzani akakimbia, akagusa mpira, akapiga shuti, wewe kama beki uwe umejitoa katika kumkabili au kukabiliana na mambo hayo kwa asilimia 100.
Itaendelea Jumamosi ijayo…