Historia itaandikwa CAF

ZIMESALIA dakika 90 tu kwa watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga kuandika historia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati zitakaporudiana na Al Merrikh ya Sudan na Power Dynamos ya Zambia wiki ijayo jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo wikiendi hii walikuwa ugenini mbele ya wapinzani wao na kila moja kufunga mabao mawili muhimu kabla ya mechi za marudiano zitakazopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo iwapo zitapenya kwenda makundi itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hizo kutinga hatua hiyo kwa pamoja na kuandika historia barani Afrika.

Yanga ikiwa jijini Kigali, Rwanda iliipasua Al Merrikh kwa mabao 2-0, huku watani wao wakilazimisha sare ya 2-2 na wenyeji Dynamos kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Mjini Ndola Zambia matokeo yaliyoziweka timu hizo katika nafasi nzuri iwapo watazitumia dakika 90 za mechi za marudiano wiki ijayo.

Yanga itaanza kurudiana na Al Merrikh Septemba 30, ikiwa imeifunga kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa kwani mwaka 1973 ilikwama kwa Wasudani hao kwa kulala jumla ya mabao 3-2 (enzi za Klabu Bingwa), kisha 2007 kwenye play-off za Kombe la Shirikisho Afrika ilitolewa kwa jumla ya mabao 2-0 kabla ya juzi kuiduwaza jijini Kigali katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Kigali Pele.

Ushindi huo mbele ya Merreikh umeiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imepita miaka 25 tangu mara ya mwisho washiriki hatua hiyo mwaka 1998.

Yanga sasa itahitaji sare yoyote, isipoteze zaidi ya bao moja au kushinda tena kwenye mechi ya marudiano.

Kwa upande wa Simba itahitaji suluhu tu kwenye pambano la marudiano litakalopigwa Oktoba Mosi au iifumue Dynamos kutinga makundi kwa mara ya tano katika misimu sita ya michuano ya CAF, huku kiungo mshambuliaji, Clatous Chama aliyefunga mabao yote mawili ya ugenini akiwakuna mashabiki wa klabu hiyo wakimjadili na kumpamba kwenye mitandao ya kijamii na katika mazungumzo yao mitaani kwa sasa.

Chama alifunga bao la kwanza juzi akiuwahi mpira wa shuti la Mzamiru Yassin lililookolewa na kipa wa Dynamos kisha kufunga jingine kwa mkwaju wa mbali akichomoa bao la pili la wenyeji na kufanya mashabiki kuwehuka juu yake wakiamini huyo ndiye Chama wanayemjua hasa kwenye mechi za aina hiyo.


REKODI KUBWA

Matokeo hayo ya juzi kwa timu zote zikicheza muda mmoja kutoka mataifa tofauti yanaweza kuzalisha historia mpya kwa klabu zote hizo kongwe kucheza hatua ya makundi kwa mara ya kwanza kwa pamoja ambalo halikuwahi kufanyika.

Mara nyingi klabu hizo zimekuwa zikipishana hata msimu uliopita Simba alipokuwa makundi ya Ligi ya Mabingwa, Yanga ilikuwa hatua kama hiyo Kombe Shirikisho na kupambana hadi kufika fainali na kulikosa taji mbele ya USM Alger kwa kuangushwa na bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.

Simba ilivuka hadi robo fainali na kutolewa kwa mikwaju ya penalti na waliokuwa watetezi, Wydad Athletic ya Morocco.


MAKALI YA KUMALIZIA

Pengine yangeweza kuwa matokeo tofauti kwa timu zote kushinda vizuri zaidi kama kungekuwa na utulivu wa kutumia nafasi ambazo walizitengeneza ndani ya mechi hizo za ugenini, kwani Yanga ilipoteza nafasi zaidi ya tano za wazi, sawa na ilivyokuwa kwa Simba mbele ya Wazambia.

Yanga ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga ila hizo tano zikiwa za wazi zaidi kutokanan na washambuliaji Clement Mzize, Kennedy Musonda pamoja na viungo, Pacome Zouzoua, Stephanie Aziz KI na Maxi Nzengeli kukosa utulivu wa kukwamisha mipira kimiani.

Al Merrikh iliucheza mchezo huo ikionekana iliisoma Yanga kwani ilijaribu kufunga njia nyingi za kutengeneza mashambulizi ya mabingwa hao wa Tanzania, lakini bado walishindwa kuhimili presha za ndani na nje ya uwanja uliokuwa umejezwa na mashabiki waliovaana rangi za jezi za Yanga, kijani na njano.

Gonjwa kama hilo pia liliitafuna Simba ugenini. Kikosi hicho cha Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwani nayo ilitengeneza nafasi nyingi za wazi na kama kuna mtu atakayejishangaa basi ni straika Jean Baleke aliyekuwa kinara wa kupoteza nafasi za wazi nyingi zikiwamo uso kwa uso na kipa wa Dynamos, Lawrance Mulenga.


SIMBA REKODI, YANGA MOTO

Simba inaonekana kama ina mlima wa kutakiwa kutengeneza matokeo ya ushindi, lakini kama kuna kitu ambacho hata ukiwaamsha muda huu kuwaambia unacheza nao wakiwa kwao, basi jasho litakutoka na kipigo utakipata kwenye uwanja wa nyumbani wa Mnyama.

Simba ina rekodi nzuri nyumbani na inajua kuzicheza mechi hizo hasa eneo ambalo watakuwa wanakabiliwa na mechi za kushikilia uhai wao, kumbuka kilichotokea kwa Al Ahly, Nkana, AS Vita, hesabu na akili kama hizo wanatakiwa kuzitumia Oktoba Mosi.

Kwa rekodi ilizonazo ni wazi, Wazambia watakuwa wanakuna vichwa hasa wakikumbuka hata kwenye pambano la kirafiki la kimataifa katika Tamasha la Simba Day, walikimbizwa na kupigwa mabao 2-0, lakini wakichungulia rekodi za Mnyama nyumbani zinawakata stimu na kujua kazi wanayo.

Yanga nayo haishikiki iko kwenye moto mkali, Al Merrikh itakapoangalia mechi za Yanga hapa nyumbani itaogopa zaidi kwani kila timu iliyocheza nayo ikiwa mwenyeji hakuna aliyetoka bila kipigo cha mabao matano iwe mechi za ligi au za kimataifa.

Yanga iliichapa Asas ya Djibuti msimu huu kwa mabao 5-1, lakini pia kwenye Ligi Kuu ikazichapa KMC na JKT Tanzania kila moja kwa kipigo cha 5-0 ambapo kwa mzuka ilionao ni wazi Al Merrikh itaweza kukutana na moto mkali katika mechi hiyo ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Kibaya zaidi ni kwamba Yanga sasa imefikisha jumla ya mechi saba za mashindano kwa msimu huu, ikifunga jumla ya mabao 21 na kuruhusu moja tu ndani ya dakika 90 za kila pambano, ikianzia Ngao ya Jamii iliposhinda 2-0 mbele ya Azam kisha kutoka suluhu na Simba katika fainali, ilipoteza kwa penalti 3-1.

Katika mechi za Ligi ya Mabingwa raundi ya kwanza ilianza na ushindi 2-0 mbele ya Asas ya Djibouti kisha ikaifumua 5-1 ziliporudiana, bao la wapinzani likifungwa kwa penalti na kwenye Ligi Kuu ilishinda 5-0 mbele ya KMC na JKT Tanzania ndipo juzi tena ikaichapa Al Merrikh kwa mabao 2-0.

Mechi ijayo ya Ligi Kuu itakuwa dhidi ya Namungo kabla ya kurudiana na Al Merrikh, michezo yote ikitarajiwa kupigwa Azam Complex kisha baada ya hapo itasafiri hadi Mbeya kuvaana na Ihefu katika mchezo mwingine wa ligi hiyo inayoongozwa kwa sasa na Mashujaa Kigoma ikiwa na pointi saba.


MSIKIE GAMONDI

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi licha ya kuwapongeza wachezaji wake amesema walistahili ushindi mkubwa zaidi ya huo dhidi ya wapinzani wao.

Gamondi alisema bado hawajamalizana na Al Merrikh na amewataka wachezaji kusahau haraka matokeo hayo na kuanza kufikiria mechi ijayo ya Ligi Kuu ikiialika Namungo keshokutwa Jumatano, kisha kurudia mchezo wa CAF.

“Tulikuwa na dakika 90 nzuri, nawapongeza sana wachezaji wangu, licha ya ugumu wa mchezo hasa kipindi cha kwanza, ila walirudi kipindi cha pili na akili kubwa ya kutafuta ushindi na tukafanikiwa, tunawaheshimu wapinzani wetu lakini nadhani tulistahili ushindi mkubwa zaidi ya huu kulingana na jinsi tulivyotengeneza nafasi za wazi,” alisema Gamondi raia kutoka Argentina.

“Mechi hii ya kwanza imekwisha, sasa tunatakiwa kuhamisha akili kwenye mechi ya ligi na baada ya hapo tutamalizana na wapinzani wetu hao wa CAF, nataka nikwambie bado hatujashinda, ushindi mzuri unatakiwa kuwa mechi hii ya pili, hata wao wanaweza kutufunga kwetu kama hatutakuwa makini.”

Kocha huyo anaisaka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza tangu mwaka 1998 kuivusha Yanga kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia kuandika historia nyingine ya kuing’oa timu ya Sudan kwenye mechi za CAF tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1969.


ROBERTINHO HUYU HAPA

Kocha wa Simba, Robertinho alisema haikuwa siku yao nzuri kwani walishindwa kupata ushindi ugenini licha ya kutengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia, ila mechi haijaisha kwa vile wana marudiano yatakayoamua timu ya kusonga mbele kwenda makundi na kikosi hicho kimepania kufanya kweli.

Robertinho alisema wanarudi na hesabu kali huku wakijipanga vizuri kwa kushinda watakapokuwa nyumbani mbele ya mashabiki wao, lakini kwanza wanatakiwa kujipanga kupunguza makosa yaliyowagharimu ugenini.

“Tumecheza vizuri, ingawa tulikuwa na baadhi ya makosa ambayo yaliwapa nafasi wapinzani wetu, nilisema kabla hii timu ni nzuri (Power Dynamos) lakini bado nafasi yetu ni kubwa tutarudi imara zaidi tutakapokuwa nyumbani,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Tutakwenda kufanyia kazi changamoto ambazo tumekutana nazo jana (juzi, Simba ni timu kubwa itatengeneza ushindi mkubwa tukiwa mbele ya mashabiki wetu.”

Kocha huyo raia wa Brazili anasaka rekodi ya kuzivusha timu kuingia makundi, kama alivyofanya na Rayon Sports 2018 na Vipers msimu uliopita, lakini akitaka kuingia katika historia ya makocha walioivusha Simba makundi ya CAF katika miaka ya hivi karibuni baada ya marehemu James Siang’a wa Kenya, Patrick Aussems na Sven Vandenbroeck kutoka Ubelgiji, Mhispania Pablo Franco na Juma Mgunda.