Hili ni Jembe

Dk.John Magufuli waziri wa ujenzi ambae ameteuliwa kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Muktasari:
Dk. Magufuli ambaye hakuwa akipewa nafasi kubwa katika mbio hizo, aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho baada ya mchakato wa nani akatwe kukamilishwa usiku wa kuamkia jana Jumapili.
KITENDAWILI cha mgombea gani wa CCM atakayepitishwa kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hatimaye kimetenguliwa baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kuteuliwa.
Dk. Magufuli ambaye hakuwa akipewa nafasi kubwa katika mbio hizo, aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho baada ya mchakato wa nani akatwe kukamilishwa usiku wa kuamkia jana Jumapili.
Baadhi ya wanamichezo wamemtaja Dk Magufuli kama Jembe baada ya kupenya kwenye mchujo uliowaacha hoi wagombea wenzake akiwamo aliyekuwa akipewa nafasi, Edward Lowassa.
Wakizungumza na Mwanaspoti wananamichezo hao wakiwamo makocha na wachezaji wa Simba na Yanga wamedai, ilikuwa lazima Dk Magufuli ashinde kutokana na uchapakazi wake na kuwa mbali na kashfa mbalimbali zilizowahi kulikumba taifa hili.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema kwa kipindi alichokuwa akimfuatilia Magufuli amegundua ni mchapa kazi haswa ambaye hataki masihara katika kazi na ni mtekelezaji. “Kuchaguliwa kwake ni kwamba, CCM haikufanya makosa kwani imemteua Jembe,” alisema Mkwasa.
Straika wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema: “CCM kupitisha Magufuli ni sawa kabisa, kwa kumfahamu kwangu najua ni kiongozi makini na yupo siriazi na kazi. Kitu anachokisimamia ni lazima akifanikishe kwa vitendo.”
Beki wa Yanga, Oscar Joshua yeye alisema kuwa: “Kuchaguliwa kwa Magufuli ni sawa kabisa kwa sababu ni jembe.”
Baadaye jana Magufuli alimteua Samiah Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.