Hii ndo Yanga bana yalipa kisasi cha miaka 20

Mchezaji Kenneth Asamoah akishangilia goli na wenzake
MICHAEL MOMBURI KENNETH Asamoah amethibitisha kwamba yeye ni profesheno. Bao lake safi la videoni dakika ya 108 limeipa Yanga Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuwanyamazisha kabisa Simba. Mashabiki wa Yanga walizidiwa kwa furaha na hata kuimba; :Hii ndo Yanga Bana'. Asamoah ambaye ni raia wa Ghana awali alikuwa akipuuzwa na mashabiki kwa madai kuwa wamesajili garasa, lakini aliondoa ubidhi alipofunga kwa kichwa krosi ya Rashid Gumbo ambaye alifanya kazi kubwa ya kuwapangua Kelvin Yondani, Juma Nyosso na Said Cholo kisha akachonga krosi ya aina yake iliyosababisha madhara yaliyowalaza mapema na kuwaziba midomo mashabiki wa Simba. Ushindi huo uliandika historia mpya kwa Yanga kwenye michuano hiyo huku Kocha Sam Timbe akiweka rekodi ya kutwaa taji hilo akiwa na klabu nne tofauti. Timbe aliwahi kutwaa taji hilo akiwa na SC Villa na Polisi Fc zote za Uganda pamoja na Atraco ya Rwanda. Hii ni rekodi ya aina yake. Katika mchezo wa jana kulikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kiwango cha soka kilichoonyeshwa na timu zote huku wachezaji wapya wakikosha mamia ya mashabiki waliofurika uwanjani hapo. Yanga ndio ilitangulia kuwasili uwanjani hapo majira ya saa 8.38 alasiri ambapo dakika chache baadaye Simba nayo ikawasili na Yanga pia ilikuwa ya kwanza kuingia uwanjani kupasha saa 9.15 na saa 9.20 Simba nao wakaingia. Simba ilianza kwa kasi mchezo huo ambapo dakika 20 za mwanzo ilitawala sehemu ya kiungo walipokuwa kwa ushirikiano mkubwa Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango na Haruna Moshi 'Boban'. Lakini dakika ya 18 Mwinyi akiwa karibu na kiungo wa Yanga Juma Seif Kijiko, aliukanyaga mwenyewe vibaya mguu wake na kumsababishia maumivu ambayo yalimlazimu kufanyiwa mabadiliko na kumuingiza Mohammed Banka ambaye mchezo ulionekana kumkataa na alishindwa kabisa kuziba pengo la Kazimoto. Kutoka kwa Mwinyi ambaye aliichezea Simba kwa mara ya kwanza, kulipunguza kasi ya pasi za kupenyeza, umiliki wa mpira na nguvu ya mashambulizi kwani Nurdin Bakar na Juma Seif walitulia kwa upande wa Yanga na kumuacha Mafisango wa Simba ahangaike pekee yake. Yanga nusura waandike bao la kwanza dakika ya saba baada ya Nadir Haroub Cannavaro kupaisha krosi ya Oscar Joshua huku Shija Mkina wa Simba akifanya hivyo tena dakika ya 12 alipopigiwa krosi na Amir Maftah. Yanga ilicheza faulo nyingi kipindi cha kwanza walipokuwa wakikabiliana na presha ya Simba ambayo iliingia kwenye boski mara nyingi zaidi lakini umaliziaji ukawa ni tatizo. Katika kipindi cha pili timu hizo zilionekana kupaniki na kucheza kwa nguvu zaidi kuliko akili jambo ambalo liliwanyima uhondo mashabiki kwani butuabutua zilikuwa nyingi kuliko ufundi. Mabeki wa Yanga Nadir Cannavaro na Chacha Marwa walifaulu kuwadhibiti Ulimboka Mwakingwe, Mussa Mgosi na Haruna Moshi ambayo walikuwa wakihangaika huku na huko. Shughuli hiyo ilifanywa pia na mabeki wa Simba Juma Nyosso na Kelvin Yondani ambao waliwabana vilivyo Davies Mwape, Jerry Tegete na Hamis Kizza. Kiiza alipachika bao dakika ya 76 kwa kichwa lakini mwamuzi Wiish Yabarow wa Somalia akalikataa kwa maelezo kuwa aliotea. Simba ilifanya mabadiliko matatu kwa kuwatoa Kazimoto, Shija Mkina na Amir Maftah na nafasi zao kuchukuliwa na Mohammed Banka, Salum Machaku na Salum Kanoni. Mabadiliko hayo hayakuisaidia Simba kwani yaliipunguza kasi, tofauti na Yanga ambayo ilipowaingia Julius Mrope, Rashid Gumbo na Asamoah kuchukua nafasi za kina Godfrey Taifa, Jerry Tegete na Juma Seif walikuwa na madhara makubwa na hata kuibuka na ushindi. DAKIKA ZIADA Timu hizo zilitoka sare dakika 90 na kuongezwa dakika 30 za ziada ambazo Asamoah alifunga bao dakika ya 108. Wachezaji walionekana kuchoka muda huo ambapo butua butua zilitawala huku mabeki wa pande zote mbili wakifanya kazi ya ziada. Ikumbukwe kuwa Simba ilikuwa na siku mbili za kupumzika tangu icheze nusu fainali dhidi ya Bunamwaya tofauti na Yanga ambayo ilipumzika siku moja tu tangu icheze na St George. KOCHA TIMBE Ameweka rekodi ya aina yake kwa kutwaa kombe hilo kwa mara ya nne. Alisema kuwa; "Ilikuwa ni kazi ngumu lakini nashukuru kwamba nimetwaa tena kombe hilo na ni zawadi kwa Yanga kwamba walichonituma kufanya nimekamilisha. "Nimewapa kombe la Ligi na sasa Cecafa. Hii fainali ilikuwa ngumu sana ila nimemaliza kazi, naangalia mambo mengine sasa, wachezaji wamejitahidi sana,"alisisitiza. Yanga sasa imenyakua kombe hilo kwa mara ya nne sawa na kocha wake Sam Timbe, ambaye amefikisha idadi hiyo ya vikombe na timu tofauti. Ilitwaa taji hilo katika miaka ya 1975, 1993, 1999 na mwaka huu. Mara mbili kati ya hizo ikiwa kwa kuwafunga watani wao Simba. Mara ya kwanza ikiwa mwaka 1975 ilipoifunga Simba 2-0 huko Zanzibar. Ilipotwaa katika miaka ya 1993 na 1999, mara zote iliishinda Villa ya Uganda. ASAMOAH Alisema; "Tulikuwa kwenye presha kubwa tangu mwanzo na kilichotakiwa ni ushindi tu na tumekamilisha, bao langu ni zawadi kwa Yanga. Ninachoweza kuwaambia mashabiki ni kitu kimoja tu wawape muda wachezaji wapya waonyeshe uwezo wao." GUMBO Mchezaji huyo aliyetoa krosi ya goli alisema; "Nafurahi ndio mechi yangu ya kwanza ya watani na nimetoa pasi nzuri, nilifanya vile kwasababu nilikuwa nje nikausoma mchezo na nikajua udhaifu watu niliokuwa nakwenda kukabiliana nao." WALIOZIMIA Mashabiki zaidi ya sita wa Simba walikuwa wakizimia hovyo jukwaani baada ya bao hilo la Asamoah kutokana na mshtuko, hata nje ya uwanja mashabiki kadhaa walionekana wamelala chini. UMEME Aibu ya aina yake ilitokea baada ya umeme kukatika wakati mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi akikabidhi zawadi kwa washindi. Gari la wagonjwa ndio lilitumika kumulika jukwaa maalumu la wageni rasmi ili zawadi zitolewe. Ilikuwa ni aibu kubwa kwani hata kituo cha SuperSport cha Afrika Kusini kilichokuwa kikionyesha mechi hizo Afrika nzima ilibidi kukatisha matangazo kutokana na umeme kukatika. BASENA Kocha wa Simba, Moses Basena alisema amesikitishwa mno kufungwa na Yanga, ambayo haitishi kwani walitawala sehemu kubwa ya mchezo na akasema kuumia kwa Mwinyi Kazimoto katika kipindi cha kwanza lilikuwa pigo kwani alilazimika kubadili mbinu baada ya kumwingiza Mohammed Banka. Simba, ambayo imetwaa taji hilo mara sita, itabidi ilijilaumu yenyewe kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi. MSHINDI WA TATU El Merreikh ya Sudan ilitwaa mshindi wa tatu baada ya kuifunga St.Georges ya Ethiopia mabao 2-0 katika mchezo wa awali uliochezwa mchana. RED SEA Katika hali isiyo ya kawaida wachezaji 13 wa Red Sea ya Eritrea iliyoondoka jijini Dar es Salaam jana Jumapili waliwaachia viongozi wao pasi za kusafiria na kutokomea kusikojulikana. Lakini habari zilizopatikana jana jioni zinasema saba kati yao walinaswa mjini Mbeya na wengine watatu walifumwa Morogoro na wanarejeshwa Dar es Salaam leo Jumatatu kujibu mashtaka.