Hesabu zaibeba Yanga Kirumba

Muktasari:

  • Jijini Mwanza, vinara Yanga watakuwa wageni wa Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya Namungo na Azam kumalizana kwenye Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa, Lindi.

Kivumbi cha Ligi Kuu Bara kinaendelea leo kwa kupigwa michezo miwili iliyobeba taswira ya mbio za ubingwa kwa msimu huu, baada ya jioni ya jana Simba kumalizana na Ihefu mjini Singida.

Jijini Mwanza, vinara Yanga watakuwa wageni wa Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya Namungo na Azam kumalizana kwenye Uwanja wa Majaliwa, uliopo Ruangwa, Lindi.

Kabla ya mechi ya jana kati ya Simba na Ihefu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida, Azam ilikuwa nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 47 baada ya mechi 21, nyuma ya Yanga yenye pointi 52 kupitia michezo 20, huku Mnyama alikuwa na pointi 45 kwa mechi 19 alizokuwa amecheza.

Timu hizo ndio pekee zinazoonekana kuwa kwenye mbio za ubingwa kulinganisha na timu nyingine 13 zilizopo katika ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16. Pia mechi za leo zitakuwa na vita nyingine ya vinara wa mabao Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam na Stephane Aziz KI ambao kila mmoja amefunga mabao 13.

Mechi hizo za leo zinazokamilisha raundi ya 22, zimebeba uzito mkubwa kwa aina ya timu zinazokutana, Yanga inakutana na Singida iliyo nafasi ya saba ikiwa na pointi 24 ambazo bado haziiweki salama katika janga la kuepuka kushuka daraja, wakati Azam na Namungo hazitofautiani sana kwa nafasi zilizopo japo Wanalambalamba msimu huu wameonekana kupania.

Tuanzie jijini Mwanza ambako watetezi Yanga watakuwa na dakika 90 za kurudisha heshima wakijua mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu walitoka kuangusha pointi tatu mbele ya Azam FC baada ya kufumuliwa mabao 2-1 katika pambano kali lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa mwezi mmoja uliopita.

Mechi tatu za Yanga zilizopita nje ya Ligi Kuu imeshinda mechi moja pekee, ikitangulia kutoa sare mbili dhidi ya Mamelodi Sundowns kisha kutolewa kwa matuta kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na iliporudi nyumbani ikashinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika Kombe la Shirikisho (FA) na kutinga hatua ya robo fainali.

HALI ILIVYO

Unaweza kusema katika mechi ya leo, Yanga ishindwe yenyewe kutokana na kiwango na matokeo yasiyoridhisha ya Singida, pia ubora wa kitimu na mchezaji mmojammoja ambao Yanga imekuwa nao katika miezi ya hivi karibuni, ni sababu zinazoiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri ugenini.

Singida imekuwa haina mwenendo mzuri katika Ligi Kuu katika miezi ya hivi karibuni na hilo linadhihirishwa na mfululizo wa matokeo mabaya ambayo imekuwa ikipata katika mechi zake tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu.

Timu hiyo katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu, imeibuka na ushindi mara moja tu, huku ikitoka sare katika mechi tatu na imepoteza sita, ikifunga mabao sita na yenyewe kufungwa 15, hali ikiwa ni tofauti kwa Yanga ambayo inaonekana haipo kileleni mwa Ligi kwa bahati mbaya kutokana na mfululizo wa matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata katika mechi za ligi na hata mashindano mengine.

Uthibitisho wa hilo unaonekana katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu ambazo Yanga imeibuka na ushindi mara nane, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja, ikifumania nyavu mara 20 na nyavu zake zikitikiswa mara tano tu.

Mwenyeji Singida Fountain Gate imekuwa haina historia nzuri dhidi ya Yanga na endapo itapata ushindi leo, itakuwa angalau imefuta machozi ya unyonge iliyonayo dhidi ya vinara hao wa ligi kwani haijawahi kupata ushindi wala sare dhidi yao tangu ilipopanda Ligi Kuu.

Katika mechi tatu zilizopita baina ya timu hizo, rekodi zinaonyesha Yanga imechukua pointi zote tisa mbele ya Singida Fountain Gate na leo ni kibarua kizito kwa wenyeji kujaribu kupindua meza mbele ya jeshi la Miguel Gamondi ambaye amekuwa akitoa dozi nene kila anapokutana na mpinzani dhaifu dhaifu.

Yanga ukiacha pointi hizo, ushindi mwembamba kwa timu hiyo mbele ya Singida ni ushindi wa mabao 2-0 wakati ule wa juu ni pale ilipoichapa timu hiyo mabao 4-1. Katika mechi hizo imefungwa mabao manane na kufunga bao moja tu.

Yanga inaingia uwanjani baada ya kutoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, huku Singida yenyewe ilichapwa mabao 3-0 na Tabora United na kutupwa kwenye michauno hiyo.

Lakini hali ni tofauti kwa Singida Fountain Gate kwani leo itaingia bila uwepo wa kocha wake mkuu, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye juzi aliiacha ghafla kambi ya timu hiyo kwa kile alichodai kuna mambo hayako sawa klabuni.

Jana katika mkutano wa waandishi wa habari, Julio aliwakilishwa na kocha msaidizi wa timu hiyo Ngawina Ngawina ambaye alisema kikosi chao kipo tayari kubadilisha historia ya matokeo baina ya Yanga.

“Yanga ina timu nzuri ndio maana unaona unaingoza Ligi, kwa hili tu kwanza lazima kuiheshimu na baada ya hapo unajipanga kuangalia namna gani utapata matokeo mbele yao, tuna wachezaji wengi wanaoijua Yanga kwahiyo tumejipanga kushinda,” alisema Ngawina.

Gamondi akizungumzia mchezo huo, japo alichekelea kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi lakini alisema bado anaamini wana kikosi kipana kinachoweza kuwapa matokeo mazuri mbele ya wenyeji wao.

“Singida ina wachezaji wazuri, tunafahamu imekosa matokeo mazuri kwenye mechi zake tano zilizopita ikishinda Moja, hatuwezi kuwadharau tunawaheshimu sana, tutaingia kwenye mchezo huo kwa hesabu za kutafuta ushindi kulingana na mpango wetu wa mechi.