Silaha mpya Yanga, Hersi aifuata Lubumbashi, ni mrithi wa Lomalisa

Muktasari:

  • Tuanze na juzi. Hersi alikuwa Uwanja wa Kibasa Maliba akitazama mchezo wa Ligi Kuu ya DR Congo Lubumbashi Sport dhidi ya TP Mazembe uliomalizika kwa suluhu.

Yanga imeanza kwa kasi mbio za usajili na safari hii haitaki kuambiwa, inapanda mwewe kujionea yenyewe ubora wa mastaa inaowataka, yaani kisasa zaidi na unavyosoma gazeti hili Rais wa klabu hiyo, Hersi Said yupo jijini Lubumbashi, DR Congo akiwafuata mastaa wawili wapya.

Tuanze na juzi. Hersi alikuwa Uwanja wa Kibasa Maliba akitazama mchezo wa Ligi Kuu ya DR Congo Lubumbashi Sport dhidi ya TP Mazembe uliomalizika kwa suluhu.

Kwenye mchezo huo Lubumbashi Sport anayoichezea beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ikicheza soka la kujilinda ikainyima ushindi Mazembe na baada ya mchezo huo Hersi alifanya kikao kifupi na Ninja akitaka kufahamu maendeleo yake lakini ziara yake ikaendelea na jana akitua kwenye mchezo mwingine mgumu.

Jana Hersi akatua Uwanja wa Victoria kutazama mechi nyingine ya Ligi Kuu nchini humo kati ya AS Union Maniema dhidi ya FC Lupopo lakini Mwanaspoti linafahamu kigogo huyo aliyeibadili Yanga kwa hesabu kali za usajili aliwafuata mastaa wawili kutoka kwenye timu zote hizo.

Pale Union Maniema, Hersi alikuwa anajiridhisha juu ya ubora wa sasa wa winga Basiala Agee ambaye ilibaki kidogo achukuliwe dirisha dogo la usajili lililopita.

Basiala ni winga ambaye anahitajika na Kocha Miguel Gamondi na Yanga ilishamalizana naye na kumwacha hapo kwa sharti anatakiwa kupewa nafasi ya kucheza na yeye mwenyewe kutunza kipaji chake.

Gamondi anataka winga mpya kwa msimu ujao baada ya kutoridhishwa na kiwango cha Msauzi, Mahlatse Makudubela Skudu ambaye kwa vyovyote Yanga itamtema mwisho wa msimu huu.

Agee ni winga anayejua kupasua ukuta wa wapinzani kwa vyenga na kupiga krosi, pia ni mzuri wa kufunga kwa mipira ya adhabu ndogo kwa mguu wa kulia.

Mbali na Basiala, pia Hersi kwa upande wa pili alikuwa na kazi ya kumtazama beki wa kushoto wa Lupopo, Chadrack Boka ambaye Yanga inataka aje kuchukua nafasi ya Lomalisa Mutambala.

Boka ambaye ni beki mrefu anayejua kupandisha mashambulizi na kuzuia, anahesabika kuwa beki bora wa kushoto na Mazembe inamtamani kila msimu lakini inajua haiwezi kumchukua kirahisi kwa kuwa ni watani wa jadi na Lupopo na hakuna biashara inayoweza kufanyika kati ya klabu hizo mbili.

Taarifa kutoka ndani ya Lupopo ni Yanga ilishabisha hodi ndani ya klabu yao ikimtaka Boka mwisho wa msimu huu, safari ambayo uhakika bosi huyo wa Yanga ametua huko kumaliza dili hilo.

Endapo kila kitu kitaenda sawa basi Yanga haitakuwa na kazi ngumu kuwapata kwani mabosi wa klabu zote ni marafiki wakubwa na tajiri wa mabingwa hao wa Tanzania, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’.

Union Maniema ina urafiki mkubwa na Yanga hatua ambayo hata Simba ilipofanya jaribio la kutaka kumsomba winga Maxi Nzengeli mchakato huo ulikwama kutokana na mawasiliano ya karibu ya Yanga na tajiri wa Maniema Generali wa Jeshi la Congo Amis Kumba.

Kumba maarufu kwa jina la ‘Tango Four’ ndiye mmiliki wa Maniema na kabla kigogo huyo kichaa wa soka alikuwa rais wa AS Vita Club na baada ya kung’atuka kwake timu hiyo ikapotea.

Hata pale Lupopo ambao ni watani wa jadi wa Mazembe tajiri wao Jacques Kyabula Katwe ambaye ni Ganava wa Jiji la Lubumbashi ni rafiki mkubwa wa GSM hatua ambayo itairahisishia Yanga kuwapata mastaa hao.