Haya ndio maneno ya Aucho kwa Hussein Kazi

Muktasari:

  • Mwanaspoti limemtafuta Kazi kutaka kujua kipi kilimliza na maneno gani aliambiwa na Aucho na Mwamnyeto baada ya kwenda kumtuliza.

BEKI wa Simba, Hussein Kazi alijikuta akilia kwa uchungu baada ya Simba kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, jambo lililowafanya Khalid Aucho na Bakari Mwamnyeto kwenda kumbembeleza na kumpa maneno ya faraja.

Mwanaspoti limemtafuta Kazi kutaka kujua kipi kilimliza na maneno gani aliambiwa na Aucho na Mwamnyeto baada ya kwenda kumtuliza.

"Nilijisikia uchungu timu yangu kufungwa kwa mabao 2-1, nikiangalia mimi ndiye niliyesababisha penalti, nikiwa kwenye harakati za kumdhibiti Aziz Ki, nikajikuta nakosa nguvu, sikujua nifanye nini," amesema.

Kazi alimchezea faulo Aziz Ki ndani ya boksi katika dakika ya 18 na staa huyo wa Burkina Faso alipiga mwenyewe penalti katika dakika ya 20 na kuipa Yanga bao la kuongoza kabla ya Joseph Guede kufunga bao la pili katika dakika 38, huku Simba ikifunga katika dakika ya 74 kupitia kwa Freddy Michael.

Kazi amesema Aucho alimwambia hakuna mchezaji asiyefanya makosa, anamuona mbali akijituma kwa bidii na kuchukulia changamoto kama somo la kumjenga.

"Aucho aliniambia nakuomba utulie, soka wakati mwingine lina matokeo ya kuumiza na yasiyotarajiwa, kasema nilicheza vizuri hakuna mchezaji asiyefanya makosa, leo yapo kwangu, kesho yanaweza yakawa kwake, Mwamnyeto alisema nikaze buti ananiona ni beki mzuri, licha ya kufungwa nimecheza vizuri," amesema na kuongeza;

"Kwa upande wa nahodha Tshabalala (Mohammed Hussein), alisema soka lina safari ndefu napaswa kuwa na moyo mgumu, kocha Seleman Matola alinipa moyo na kunishika mkono kuniondoa uwanjani."