Hawa mastaa wa kimataifa waliobeba ndoo Ligi Kuu Bara

Muktasari:
Hata hivyo, makala haya yanaangazia nyota ambao walikuja kwa nia moja tu, kubeba mataji na hadi wanamaliza soka lao nchini hawajaondoka patupu.
TANZANIA ni moja ya nchi za Afrika Mashariki ambayo imekuwa ikikimbiliwa na nyota wengi wa kimataifa. Hii ni kwa sababu soka nchini lina mashabiki wengi na biashara yake inakua kwa kasi.
Nyota kibao wa kimataifa wameshakuja na kuondoka. Wapo walioondoka wakiwa vinara wa kupachika mabao, viungo bora, makipa bora na hata kwenye safu ya beki, wapo waliotisha na kuwafunika wazawa.
Hata hivyo, makala haya yanaangazia nyota ambao walikuja kwa nia moja tu, kubeba mataji na hadi wanamaliza soka lao nchini hawajaondoka patupu.
HARUNA NIYONZIMA 5
Kiungo huyu mshambuliaji Mnyarwanda ni miongoni wa wachezaji wa kigeni waliocheza kwa mafanikio. Niyonzima alitua nchini 2011/12 akitokea APR. Ndiye mchezaji aliyenyanyua makwapa mara nyingi zaidi kwa nyota wa kigeni kuanzia msimu aliotua.
Amecheza misimu sita Yanga na kutwaa taji mara nne akianzia mwaka 2013, baadaye akatwaa taji mara tatu mfululizo kuanzia 2015, 2016 na 2017, kabla ya kutimkia Simba na huko akalitwaa mara mbili mfululizo 2017 na 2018.
Kwa sasa nyota huyo aliyekuwa kipenzi cha mashabiki nchini kutokana na ufundi wake hadi kufananishwa na nyota wa zamani wa Barcelona na Arsenal, Cesc Fàbregas amerudi nchini kwao baada ya kumaliza mkataba na Simba na sasa anakipiga AS Kigali.
AMISS TAMBWE 4
Ni mshambuliaji aliyecheza Simba na Yanga na ameweza kutwaa mataji akiwa na timu hizo akianza na Simba mzimu wa 2013/14 na kufanikiwa kutwaa kiatu cha dhahabu akiibuka mfungaji bora.
Tambwe ambaye ameachwa baada ya kumaliza mkataba wake alipotua Yanga, pia alifanikiwa kutwaa taji ikiwa ni sambamba na kiatu cha dhahabu msimu wake wa kwanza tu kutua Yanga akifanya hivyo mara tatu mfululizo mwaka 2015, 2016 na 2017.
THABAN KAMUSOKO 2
Aliwahi kuifunga Yanga akiwa katika timu yake ya FC Platinum katika Kombe la Shirikisho kwa faulo na kuwashawishi mabosi wa Jangwani kufunga safari ya kumfuata nchini kwao kwa ajili ya kumleta Tanzania. Agosti 6, 2015 waliinasa saini yake.
Akiwa katika klabu ya Yanga na kufanikiwa kutwaa taji msimu wake wa kwanza, alikiri kutwaa taji lake la kwanza tangu ameanza kucheza soka la ushindani, na kwa bahati hiyo hakuishia hapo aliendelea kuipambania timu na kufanikiwa kutwaa taji lingine msimu uliofuata.
Kamusoko sasa ametimkia nchini Zambia ambapo anakipiga katika klabu ya Zesco chini ya kocha wake wa zamani ambaye alifanya naye kazi wakiwa Yanga, George Lwandamina.
EMMANUEL OKWI 2
Okwi ni kipenzi cha wana Simba. Ukitaka kutukanwa, basi mtolee maneno machafu mshambuliaji huyo mbele ya mashabiki wa Msimbazi, ni kutokana na umahiri wake ikiwa ni sambamba na kuwa na mapenzi na timu hiyo kwani amekuwa mtu wa kucheza na kuondoka. Nyota huyu amecheza timu mbili hasimu - Simba na Yanga.
Misimu miwili iliyopita ndio ilikuwa ya mafanikio makubwa kwake baada ya kuiongoza Simba kutwaa mataji mawili na kuibuka mfungaji bora ndani ya msimu mmoja waliotwaa taji kabla ya Meddie Kagere hajatua na kufanikiwa kutwaa kiatu hicho msimu uliofuata.Okwi ambaye sasa ametimkia Al-Ittihad ya Jiji la Alexandria nchini Misri, alitwaa mataji mawili akiwa Simba katika msimu wa 2017 na 2018.
JAMES KOTEI 2
Kotei aliwasili nchini Desemba 2016 akitokea kwao Ghana na alikuja kufanya majaribio katika kikosi cha Simba kilichokuwa kambini Morogoro.
Alifanya majaribio ya wiki moja na wekundu hao huko Morogoro na kocha wa wakati huo, Joseph Omog alilipitisha jina lake na kuwaambia viongozi wamsajili kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo. Uongozi wa Simba ulikubaliana na hilo hasa baada ya kuonyesha soka safi kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex na kumpa mkataba wa mwaka mmoja.
Kotei ameitumikia Simba kwa misimu mitatu na ametwaa makombe manne huku akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kombe lake la kwanza lilikuwa la FA katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma walipoifunga Mbao FC mabao 2-1. Kombe hilo liliipa Simba nafasi ya kwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukosa mechi za kimataifa kwa misimu minne.
Kotei akiwa na Simba ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo baada ya timu yake kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mitano. Pia alichukua ubingwa wa Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
ASANTE KWASI 2
Desemba 15 kabla dirisha dogo la usajili halijafungwa Simba ilinasa saini ya mchezaji wa zamani wa Lipuli FC, Mghana Asante Kwasi anayemudu vyema nafasi ya ulinzi na kiungo mkabaji.
Mchezaji huyo alinaswa kwa mkataba wa miaka miwili na mabosi wa Simba walivutiwa na uhodari wake wa kukaba na kushambulia. Hadi anatimka Tanzania alifanikiwa kufumania nyavu mara nane, sita akifunga akiwa nje ya Simba na mawili aliifungia Lipuli FC.
Kwasi sasa anakipiga katika klabu ya Baroka FC baada ya kumaliza mkataba na Simba akiwa ametwaa mataji mawili mfululizo katika msimu wa mwaka 2017 na 2018.
DONALD NGOMA 2
Kocha Hans Van Pluijm ndiye aliyetoa pendekezo kwa viongozi kunasa saini ya Ngoma ambaye alikuja Tanzania kucheza na Yanga akiwa FC Platinum, lakini hakupata nafasi ya kucheza Uwanja wa Taifa na baadaye kuisumbua safu ya ushambuliaji ya Yanga nchini Zimbabwe.
Pluijm alimuangalia mshambuliaji huyo katika mchezo wao wa marudiano na kuomba uongozi umsajili ambapo haukufanya ajizi ulimnasa katika msimu wa 2015/16 akisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili. Ndani ya usajili wa misimu hiyo Ngoma aliiongoza Yanga akiwa mshambuliaji wa kutegemewa na kuisaidia kutwaa mataji mawili mfululizo kabla hajatimkia Azam FC ambako ndiko anakipiga kwa sasa.
NICHOLAUS GYAN 2
Mshambuliaji huyu kutoka Ghana alisajiliwa msimu wa 2016 akitokea klabu ya Ebusua Dwarfs ya Ligi Kuu Ghana alijiunga na timu hiyo kama mshambuliaji, lakini baadaye alibadilishwa majukumu kutokana na safu ya ushambuliaji kukamilika.
Gyan alijikuta anachezeshwa kama beki chini ya kocha Pierre Lechantre ambaye baada ya kutimka Tanzania mchezaji huyo hakuwa na namba kwenye kikosi cha Patrick Aussems hadi mkataba wake ulipoisha na kuamua kutimka.
Gyan ametwaa mataji mawili akiwa chini ya kocha Aussems.
JUUKO MURSHID 2
Ni beki wa timu ya Taifa ya Uganda aliyejiunga na Simba 2014. Ni miongoni mwa makeki bora wa kimataifa ambaye amecheza misimu mingi zaidi katika timu hiyo na baadaye kupoteza namba kikosi cha kwanza.
Akiwa ni chaguo la kwanza timu ya Taifa ya Uganda, nyota huyo hakuwa na namba kwenye kikosi cha Aussems na kuamua kutimkia nchini kwao huku akiomba mkataba uvunjwe. Murshid ameondoka Simba akiwa hajamaliza mkataba na kuamua kujiunga na Wydad Casablanca ya Morroco akiwa tayari ametwaa mataji mawili mfululizo chini ya Aussems.