Hatma ya Morrison, Mkude mwezi huu

Muktasari:
Kwa upande wa viongozi, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amepelekwa kwenye kamati hiyo kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari na kauli za maudhi kwa viongozi wa Polisi Tanzania.
KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), mpaka sasa inasubiriwa kutoa uamuzi wa wachezaji wawili pamoja na viongozi watano waliopelekwa kwenye kamati hiyo kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
Wachezaji wanaosubiri kuitwa na kamati hiyo ni Jonas Mkude wa Simba na Bernard Morrison wa Yanga ambao walipelekwa Februari 22 na 26 kabla ya mchezo wa watani wa jadi uliopigwa Machi 8.
Mkude amepelekwa kwenye kamati hiyo kutokana na madai ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United FC katika mchezo uliofanyika Februari 22, Uwanja wa Taifa na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Naye nyota wa Yanga, Morrisson alikutwa na kosa kama hilo kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma Februari 15, huku mchezo ukiwa umesimama.
Kwa upande wa viongozi, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amepelekwa kwenye kamati hiyo kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari na kauli za maudhi kwa viongozi wa Polisi Tanzania.
Bwire alikumbwa na mkasa huo katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, Februari 22 na Polisi Tanzania kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Pia viongozi wa Mtwivila FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL), meneja wa timu, Omary Albert; Katibu Oscar Mkusa na Kocha Mkuu Petro Mrope kwa pamoja wamepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kosa la udanganyifu wa leseni ya mchezaji, Christopher Rashid Kidava.
Viongozi hao walifanya kosa hilo katika mechi iliyochezwa Februari 29, 2020 katika Uwanja wa Mkwawa mkoani Iringa dhidi ya Tukuyu Stars na timu hizo kutoka suluhu, lakini baada ya maamuzi Tukuyu walipewa alama tatu.
Hata hivyo, Katibu wa Kamati ya Nidhamu, Herman Kidifu amesema wanatarajia kukutana mwishoni mwa mwezi kuwajadili wachezaji na viongozi waliopelekwa kwenye kamati hiyo.
“Tunapenda kufanya maamuzi haraka, lakini changamoto zinazotukabili ndio zinasababisha kuchelewa kidogo kukutana kwa haraka na kufanya maamuzi kwa wale wanaoletwa kwenye kamati,” aliema Kidifu.