Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hapa Simba ishindwe wenyewe tu

Muktasari:

  • Faida hiyo ni kuanza msimu ikiwa haina mabadiliko makubwa katika benchi lake la ufundi kulinganisha na Yanga na Azam ambazo zenyewe zimejikuta zikiwa  na kundi kubwa la maofisa wapya wa mabenchi yao ya ufundi kutokana na wale waliokuwa wakiyaongoza hapo awali kuachana na timu hizo

SIMBA ina kibarua cha kufanya usajili wa idadi kubwa ya wachezaji kulinganisha na Yanga na Azam FC, lakini ina faida moja ambayo ikiitumia vyema inaweza kuwazidi kete wahindani wake hao wawili.

Faida hiyo ni kuanza msimu ikiwa haina mabadiliko makubwa katika benchi lake la ufundi kulinganisha na Yanga na Azam ambazo zenyewe zimejikuta zikiwa  na kundi kubwa la maofisa wapya wa mabenchi yao ya ufundi kutokana na wale waliokuwa wakiyaongoza hapo awali kuachana na timu hizo.

Wakati mabenchi mapya ya Yanga na Azam yakiwa na kibarua cha kuizoea ligi lakini pia wachezaji ambao watawafundisha kwa msimu ujao, hali ni tofauti kwa Simba ambayo benchi lake la ufundi linaonekana kutoanza upya kutokana na uzoefu lililonao kwa ligi na wachezaji waliopo.

Katika benchi la ufundi la Simba, mabadiliko yaliyofanyika ni ya meneja mpya wa timu, kocha mpya wa mazoezi ya viungo kwa wachezaji na kocha wa makipa huku nafasi nyingine zikiwa na sura ambazo sio ngeni.

Kocha wa makipa mpya ni Daniel Cadena aliyechukua nafasi ya Chlouha Zakaria wakati kocha mpya wa mazoezi ya viungo ni Corneille Hategekimana anayechukua nafasi ya Kelvin Mandla na pia imemuajiri Mikael Igendia kuwa meneja wa timu akirithi nafasi ya Patrick Rweyemanu ambaye kwa sasa anahudumu kama Mkuu wa Programu za Vijana ndani ya klabu hiyo.

Lakini licha ya upya wa hao ndani ya timu, Simba ina jeuri ya uwepo wa kocha mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho' ambaye ana uzoefu mkubwa wa mashindano ya klabu Afrika lakini pia hata ule wa mashindano ya ndani kwani tayari ameshaiongoza Simba katika mechi 10 za Ligi Kuu msimu uliomalizika.

Ukiachana na uzoefu huo wa ligi,timu na mazingira ambao Robertinho anao, faida nyingine kwa Simba ni kwamba hata nyota wapya wanaosajiliwa wametokana na mapendekezo yake jambo linaloashiria anawafahamu vyema.
Ukiondoa Robertinho, Simba pia imeonekana kujiweka katika mazingira mazuri ya kunufaika kutokana na kumbakisha kocha msaidizi Juma Mgunda ambaye amekuwa na uzoefu mkubwa na soka la ndani.

Kazi kubwa inaonekana kuwa kwa Yanga na Azam ambazo mabenchi yao ya ufundi yatakuwa na kibarua kigumu cha kumudu mazingira ya Tanzania kutokana na ugeni wao.

Yanga yenyewe ina kocha mkuu mpya ambaye ni Miguel Gamondi lakini pia hata kocha msaidizi italazimika kusaka mpya baada ya kuachana na Cedrick Kaze na italazimika kusaka kocha mpya wa makipa baada ya kuagana na milton Nienov.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, pia wako katika uwezekano wa kumpoteza mtaalam wa mazoezi ya viungo, Helmi Guedrich.
Wakati ikiwa hivyo kwa Yanga, Azam nayo itakuwana benchi jipya la ufundi litakaloongozwa na Youssouph Dabo na msaidizi wake Bruno Ferr.

Maofisa wengine wapya wa benchi la ufundi la Azam FC ni Khalifa Ababakar Fall ambaye ni kocha wa makipa, Ibrahim Diop (mchambuzi wa viwango) na Jean-Laurent Geronimi atakayehudumu kama mtaalam wa mazoezi ya viungo vya mwili.
Kocha wa Makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alisema kutokuwepo kwa mabadiliko ya  makocha kwa upande wa Simba hakuwapi nafasi ya wao kufanya vizuri msimu ujao kwani bado kocha ana kibarua kizito cha kuwasoma wachezaji wapya na kufanya nao kazi ijapokuwa baadhi yao watakuwa wenyeji.

"Msimu ujao kwa pande zote hautakuwa rahisi kwani kila mahala pana changamoto mpya ila kwa upande wa Simba kutobadilisha makocha hakuwapi nafasi ya kufanya vizuri," alisema Kocha Mwangata.
Mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said, alisema Yanga wana kazi ya ziada kwani kocha hawajui wachezaji vizuri hivyo mwanzo lazima wapate shida kidogo kama ilivyokuwa kwa Simba.

"Yanga itakwenda kupitia changamoto kidogo mwanzoni kama Simba kwani kocha atakuwa mgeni hivyo kila kitu kitaanza upya hata kama wana wachezaji wenye ubora kiasi gani," alisema Dua.