Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gusa achia ilivyoibeba Yanga kwa TP Mazembe

Muktasari:

  • Ni kweli Yanga ilianza kichovu mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi A kwa kupoteza michezo miwili mfululizo, ikilala 2-0 nyumbani mbele ya Al Hilal ya Sudan kisha idadi kama hiyo ilipokuwa ugenini dhidi ya MC Alger ya Algeria, lakini kasi ilibadilika ilipocheza mechi ya kwanza dhidi ya Mazembe jijini Lubumbashi.

WALE waliokuwa wakiiponda Yanga ya Sead Ramovic kwamba haina kitu, kwa sasa huenda wanatafuta mahali pa kuficha sura zao, kwa namna Gusa Achia Twende Kwao ilivyoanza kulipa kwa kikosi hicho kuzitaabisha timu pinzani, kama ilivyofanya juzi kwa TP Mazembe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ni kweli Yanga ilianza kichovu mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi A kwa kupoteza michezo miwili mfululizo, ikilala 2-0 nyumbani mbele ya Al Hilal ya Sudan kisha idadi kama hiyo ilipokuwa ugenini dhidi ya MC Alger ya Algeria, lakini kasi ilibadilika ilipocheza mechi ya kwanza dhidi ya Mazembe jijini Lubumbashi.

Ikichagizwa na ushindi wa mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara, Yanga ya Ramovic imekuwa ya moto na TP Mazembe wanaweza kuwa mashahidi wazuri katika mchezo wa marudiano uliopigwa juzi Kwa Mkapa, ambao timu hiyo ya DR Congo ilikumbana na aibu ya kupigwa mabao 3-1 ikiwa ni kipigo kikubwa kwao kwa msimu huu katika hatua ya makundi.

Sio kufungwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyowahi kufanyiwa mwaka 2023 katika hatua kama hiyo ya makundi lakini kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, pia ilipigiwa mpira mwingi hasa kipindi cha pili na kuwavuruga kabisa, tofauti na ilivyocheza kwenye mchezo wa kwanza ilipokuwa nyumbani DR Congo katika sare ya 1-1.

Yanga ilipata ushindi huo na kufufua matumaini ya kucheza robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo, kwani imefikisha pointi nne kama ilizokuwa nazo MC Alger ambayo usiku wa jana ilikuwa ugenini kumalizana na vinara wa kundi hilo, Al Hilal.


45 ZA KWANZA

Katika mchezo huo wa juzi ambao ulishuhudiwa dakika 45 za kwanza zikimalizika kwa sare ya 1-1, Yanga ilipaswa kujilaumu kwa kushindwa kupata uongozi wa mabao mengi kwa jinsi ilivyopoteza nafasi nyingi za wazi.

Kilichoitiobulia Yanga ni aina ya pasi ilizokuwa ikipiga kwenda katika lango la Mazembe, huku eneo la kiungo na washambuliaji wakikosa utulivu uliozoeleka au ulioonekana katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara ambapo Yanga ilishinda kwa idadi kubwa ya mabao dhidi ya TZ Prisons, Dodoma Jiji na Fountain Gate.

Shukrani pekee ni utulivu na akili aliyoipata Clement Mzize aliyepokea pasi ya Chadrak Boka na kuamua kupiga shuti kali la mbali lililotinga wavuni kuisawazishia Yanga bao baada ya wageni kutangulia kwa mkwaju wa penalti ya dakika ya 16 ilipigwa na kipa Badara Fatty aliyemtungua Diarra Djigui aliyerejea uwanjani akitoka majeruhi.


GUSA ACHIA MOTO

Kipindi cha pili ndicho kilichoonyesha Yanga na Ramovic ina rangi gani pengine baada ya wachezaji kukumbushwa kwamba wakipoteza mchezo huo, wajue kabisa robo fainali wataisikia hewani na kurudi na moto mkali wa kuonyesha Gusa Achia inachezwaje na kuwazima wapinzani wao.

Yanga ya kipindi cha pili ilikuwa hatari zaidi hasa kutokana na utulivu wa Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Prince Dube pamoja na ufundi na akili za kibabe za Mzize walioichachafya ngome ya Mazembe iliyokuwa imefanya mabadiliko kadhaa ili kupunguza presha kubwa ya wenyeji.

Gusa Achia ilizalisha mabao mawili ya kiufundi kama ilivyokuwa la kwanza la Mzize katika kipindi cha kwanza, japo mabao yote hayo hakuna lililotengenenezwa kwa pasi zaidi ya nne, isipokuwa ilipigwa kati ya pasi mbili na nne tu kisha chuma kinakaa kambani.

Hata bao la kwanza la Yanga, lilitokana na soka la haraka kwenda lango la wapinzani na Mzize kufunga akitumia pasi mbili tu yaani mpira kutoka kwa beki Ibrahim Bacca aliyempasia Boka aliyeugawa kwa mfungaji huyo naye akamalizia wavuni kwa shuti kali la mbali.


Bao la pili nalo Yanga ikatumia pasi nne tu kufika lango la Mazembe na Aziz KI akafunga kwa utulivu akiupitisha katikati ya miguu ya kipa Fatty, baada ya kupokea pasi na Khalid Aucho ambaye ndiye aliyeanzisha shambulizi hilo.

Kwa bao la tatu la Yanga, hali ilijirudia ikipiga pasi mbili tu kufunga bao lililofungwa na Mzize, ikiwa na maana ile falsafa ya soka lao iliyopewa jina la Gusa Achia Twende Kwao iliyoletwa na kocha Ramovic imeingia katika damu ya wachezaji wa timu hiyo na kuendelea kuwatesa wapinzani.


ZEMANGA ALITIBUA

Mazembe kama kuna kitu kiliifurahisha Yanga ni baada ya kutolewa kwa kiungo Zemanga Soze ambaye hata bao walilotengeneza lilikuwa na mchango wake ambapo kila alipokuwa anagusa mpira kuelekea lango la wenyeji alikuwa hatari kwa pasi zake za kibabe na kiufundi ambapo baada ya kupumzishwa timu yake ilipata shida katikati.

Mchezaji huyo alionekana kuwa tishio langoni mwa Yanga, hivyo kutolewa kulikuwa nafuu kubwa kwa wenyeji na kupata muda wa kutembeza boli kwa mtindo ule wa gusa achia twende kwao na ikalipa Kwa Mkapa.


MJIPANGE

Kama kuna timu  inatarajia kukutana na Yanga, isithubutu kusema zilizofungwa ni wachovu, kwani ukweli Yanga ya sasa inacheza kwa kasi kubwa na ina pumzi ya kutosha mwanzo mwisho na juzi ilionekana Kwa Mkapa tofauti na Yanga iliyoanza mechi za awali za makundi.

Mazembe ni mashahidi, ilikutana na kitu kizito tofauti na zilipokutana Desemba 14, mwaka jana pale Lubumbashi, kwani katika mchezo wa juzi Yanga kwenye kila shambulizi lililoenda kutengeneza bao ilitumia soka la haraka sana tena wakiwa wachache dhidi wengi wa Mazembe ambapo bao la kwanza wachezaji wa wenyeji walikuwa sita dhidi ya wanane kwenye eneo la Mazembe hadi Mzize anafunga bao hilo.

Bao la pili tena Yanga ilikuwa na wachezaji wanne dhidi ya saba wa Mazembe na hata bao la tatu Yanga ilikuwa na watu watano dhidi ya wanane wa TP.

Mazembe haikujua ikabe vipi lakini hata wakati inashambuliwa haikuwa na kasi ya kuhakikisha inapokonya mpira kwa haraka na kuipa nafasi Yanga kutawala mchezo huo ikipiga mashuti 20 huku manane yakilenga lango, wakati Mazembe iliambulia mashuti matatu tu yaliyolenga lango kati ya tisa iliyopiga. Mazembe iligongesha nguzo mara mbili kwa mipira ya kutengwa na mtokea benchini wa TP alibaki na kipa tu, lakini alikosa umakini shuti lake dhaifu likadakwa na Diara, ikiwa ni taa nyekundu kwamba wageni licha ya kutokuwa na mchezo mzuri bado wangeweza kufunga hadi mabao manne juzi.


KIBWANA HATARI SANA

Kibwana Shomari, ambaye hakuwa na nafasi katika kikosi cha kocha aliyeondoka, Miguel Gamondi, alicheza kwa kiwango cha juu sana akimnyima nafasi ya kufurukuta, winga hatari zaidi wa Mazembe, Oscar Kabwiti, ambaye alilazimika kupumzishwa katika dakika ya 70 baada ya kupotezwa kabisa na beki huyo wa Morogoro. Kocha Ramovic alionekana akimkumbatia kwa furaha Kibwana baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.

KAZI IPO MAURITANIA

Yanga sasa ina kibarua katika mechi ijayo wikiendi hii ugenini dhidi ya Al Hilal kabla ya kurudi nyumbani Januari 18 kuikaribisha MC Alger Kwa Mkapa.