GSM akagua eneo la uwanja wa Yanga Jangwani
Muktasari:
- Kikao hicho ambacho kimefanyika jana asubuhi Makao Makuu ya Klabu ya Yanga mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, kimewajumuisha wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo wakiongozwa na Rais, Injinia Hersi Said na Makamu wake Arafat Haji.
UONGOZI wa Yanga, umefanya kikao cha mwisho juu ya ujenzi wa uwanja wa timu hiyo, huku mfadhili na mshindi wa zabuni ya tenda hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ akitembelea eneo la mradi.
Kikao hicho ambacho kimefanyika jana asubuhi Makao Makuu ya Klabu ya Yanga mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, kimewajumuisha wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo wakiongozwa na Rais, Injinia Hersi Said na Makamu wake Arafat Haji.
Mbali na viongozi hao wa Yanga, pia wamekuwepo kamati ya ujenzi huo ukiongozwa na Mwanasheria Alex Mgongolwa pamoja na upande wa kampuni iliyoshinda zabuni hiyo akiwemo GSM mwenyewe.
Mara baada ya kikao hicho kumalizika, GSM alitembelea eneo la ujenzi wa uwanja huo ambalo awali ulikuwa Uwanja wa Kaunda na kujionea ukubwa na mipaka yake.
Hersi na Arafat walionekana kumpa taarifa mbalimbali juu ya eneo hilo ambapo baada ya hapo GSM alimaliza ziara hiyo kwa maneno mafupi akisema: “Basi nadhani inatosha, nimejiridhisha.” Kisha akaagana na viongozi hao na kuondoka eneo hilo.
Baada ya ziara hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kikao hicho kimekamalisha taratibu zote za awali kwenye mchakato wa ujenzi wa uwanja huo.
Kamwe amesema kila kitu kuhusu makubaliano ya ujenzi wa uwanja huo kutoka pande hizo mbili yamekamilika na Ijumaa Mei 15, 2026 kutakuwa na hafla maalum ya kusaini mkataba pamoja na kuweka wazi tarehe ya ujenzi huo utakapoanza.
“Leo tumekuwa na siku muhimu kweli ambayo tunaweza kuiita siku ya kihistoria, taarifa nyingi za kina zitakuja kuzungumzwa baadaye, kilichojadiliwa ndio kimebeba historia,” amesema Kamwe.
“Ukiangalia mchakato mzima kuanzia ulipoanza, klabu ya Yanga kutangaza kampuni mbalimbali kuomba kushirikiana na uongozi wa klabu yetu, kampuni mbalimbali kuwasilisha maombi na baadaye kupatikana GSM kuwa ndio washindi.
“Baada ya hapo uongozi ukaunda kamati itakayosimamia mchakato huo, vikafanyika vikao vingi lakini leo (jana) tukafikia kwenye kikao cha mwisho kati ya uongozi wa Yanga na mshindi wa zabuni, nasema cha mwisho kwa kuwa ndio kikao cha makubaliano namna gani sasa pande hizi mbili zinashirikiana.
“Kuanzia kwenye umiliki wa huo uwanja, gharama zitakuwaje, uwanja utaanza lini kujengwa, kila kitu kimekamilishwa leo, taarifa za kina zilikuwa tuzitoe leo (jana) lakini kama mnavyofahamu uongozi upo kwenye harakati za mchezo wa kesho (leo dhidi ya Dodoma Jiji) sasa tumekubaliana kutakuwa na hafla maalum Ijumaa ambayo sasa kila kitu kitawekwa wazi pamoja na pande hizi mbili kusaini mkataba wa ushirikiano.”