GSM aisapraizi Yanga Arusha

MFADHILI wa Yanga Ghalib Said Mohammed 'GSM' amewafanyia sapraizi wachezaji wa timu hiyo baada ya kutua kimyakimya jijini Arusha kushuhudia mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho la Azam.
Yanga leo itakuwa na fainali ngumu dhidi ya Coastal Union isiyotabirika,mchezo utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani humo.
Wakati presha ya mchezo huo ikizidi kuongezeka GSM ametua jijini Arusha jana usiku kimyakimya tayari kwa kushuhudia mchezo huo.
Hii ni mara ya pili kwa GSM kuishuhudia Yanga ikicheza fainali ambapo mara ya mwisho aliishuhudia timu hiyo ikiwachapa Simba kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar huku Yanga ikichukua taji hilo.
Katika Fainali hiyo iliyopigwa Januari 13 Yanga iliishinda kwa penalti 4-3 na kuchukua taji hilo mbele ya watani wao wa jadi.
Taarifa za ndani ya Yanga zinasema GSM tayari ameshawapa ahadi ya sh 200 milioni wachezaji wa timu yake kama watachukua taji hilo.
Endapo Yanga itachukua taji hilo watakuwa wamekamilisha kuyapokonya mataji yote matatu kutoka Tanzania Bara baada ya awali kukamilisha kuchukua Ngao ya Jamii na Ubingwa wa Ligi Kuu Bara.