Gomes awazidi ujanja waarabu

KIKOSI cha Simba kinashuka uwanjani leo kumalizana na Dodoma Jiji katika Ligi Kuu Bara, lakini Kocha Mkuu wake, Didier Gomes amefanya jambo moja kubwa akiwazidi ujanja Waarabu wanaotarajiwa kukutana nao kwenye mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo kutoka Ufaransa akijua amesaliwa na mechi nne tu za michuano ya ndani kabla ya kuanza jukumu lake kimataifa, ameamua kuwatumia marafiki zake waliopo katika nchi za Algeria na Afrika Kusini zinazotoka timu ambazo inaweza kupangwa nao za MC Alger na CR Belouizdad za Algeria na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini sambamba na kuwasoma mapema kupitia video.

Simba ina mechi tatu za ligi ukiwamo wa kesho dhidi ya Dodoma Jiji, kisha kuvaana na watani wao, Yanga Mei 8 na ile ya Wagosi wa Kaya, huku ikiwa pia na mchezo wa Kombe la ASFC dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kuanza vita Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya droo itakayofanyika Ijumaa hii.

Katika mechi hizo za CAF zitakazoanza kupigwa kati ya Mei 14-22 kutafuta timu nne za kucheza nusu fainali ya michuano hiyo, Simba ina uwezekano mkubwa wa kupangwa na moja ya timu hizo tatu na Kocha Gomes amejiongeza kwa kuanza kuwasoma wapinzani wao mapema ili asipate tabu akikutana nao.

Simba itaanzia ugenini katika mechi zao hizo za CAF kisha kumalizia kazi nyumbani na Gomes ameanza maandalizi mapema kwa kuwasoma wapinzani wake kupitia video za mechi zao pamoja na kuwatumia marafiki zake wanaoishi kwenye nchi zinazotoka timu hizo ili kuwasoma vyema.

Hata hivyo, Gomes alisema angependa kupata matokeo mazuri kwenye michezo yao ya ndani kabla ya kuanza kuwafikiria wapinzani wao wa CAF, lakini mpaka sasa ameshawasoma vya kutosha Wasauzi na Waarabu kupitia marafiki zake wanaompa dondoo zao kwa undani.

“Tunatumia mechi hizo za mashindano ya ndani ili kujiandaa na mechi za kimataifa kwani tukifanya vizuri maana yake hali na morali ya kushindana kwa wachezaji inakuwa kubwa ifikapo mchezo huo,” alisema Gomes na kuongeza kuwa, Afrika Kusini na Algeria kuna wataalamu wa soka ambao anafahamiana nao kuna vitu vya kiufundi ambavyo anavichukua kutoka kwao ili kuhakikisha yeyote ambaye watakutana naye wanakuwa tayari kwa kumkabili.

“Unajua mechi kubwa kama hizo za robo fainali zinahitaji maandalizi ya kutosha tena ya mapema ndio maana hata kwa upande wangu nimelifanya hilo ili kuhakikisha tunafikia malengo ambayo tumejiwekea,” alisema Gomes na kuongeza;

“Kuna kanda za video mbalimbali zinazoonyesha mechi za timu hizo tatu ambazo mmojawapo naweza kukutana nayo na tumekuwa tukizichambua kitaalamu. Kuna vitu vingi vya kiufundi ambavyo tumegundua kutoka kwao na tutavifanyia kazi ili kuwa kama silaha kwa upande wetu, sina wasi wasi nina imani tunaenda kufanya vizuri na tutaweka rekodi ya kufika nusu fainali.”

Kama Simba itafanikiwa kutinga nusu fainali itakuwa wameirejea tena rekodi yao ya mwaka 1974 walipotinga hatua hiyo wakati michuano ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika kwa kufungwa kwa mikwaju ya penalti na Mehalla Kubra ya Misri baada ya kushinda 1-0 nyumbani na kulala 1-0 ugenini.