Genk wamekunja Sh89 Bilioni za usajili wa Samatta kwenda Aston Villa wametulia

Muktasari:

Genk imekunja Pauni 8.5 milioni kwa mauzo ya Samatta. Ilimnunua kwa dau la Euro kama 200,000 hivi kutoka kwa Moise Katumbi pale TP Mazembe katika dirisha la Januari 2006. Ilitazama pia namna ya kumuuza katika siku za usoni na sio awapatie ufalme wa mataji tu.

WAKATI Watanzania wakiwa wanafurahia kumuona Mtanzania Mbwana Samatta akivaa jezi ya Aston Villa katika Ligi kuu ya England ni wakati wa kutafakari mambo mengine. Labda ni wakati wa kuitafakari klabu yake aliyotoka.
Kuna maisha mengine yanaendelea kule katika klabu yake aliyotoka. Genk. Umetafakari biashara waliyofanya katika dirisha dogo la Januari ambalo lilimuona Samatta akiondoka kwao na kwenda katika Ligi Kuu ya England?
Genk imekunja Pauni 8.5 milioni kwa mauzo ya Samatta. Ilimnunua kwa dau la Euro kama 200,000 hivi kutoka kwa Moise Katumbi pale TP Mazembe katika dirisha la Januari 2006. Ilitazama pia namna ya kumuuza katika siku za usoni na sio awapatie ufalme wa mataji tu.
Na sasa imemuuza kwa faida kubwa. Pauni 8.5 milioni kibindoni. Lakini hapohapo imemuuza kiungo wa kimataifa wa Norway, Sander Berge ambaye alikuwa anang’ara klabuni hapo kwa dau la Pauni 22 milioni kwenda Sheffield United, pia ya Ligi kuu ya England.
Dau la Pauni 22 milioni ni rekodi kwa Sheffield. Haijahi kumnunua mchezaji kwa dau hilo. Unaweza kujiuliza kwanini Genk imepata pesa nyingi zaidi kwa Berge kuliko Samatta wakati Samatta alikuwa staa zaidi ukweli ni kwamba Berge ana umri mdogo.
Berge ana umri wa miaka 21 tu. Timu kubwa za Ulaya zilishaanza kumtolea macho kutokana na uraia wake pamoja na umri wake. Miaka 21 halafu Mzungu. Huyu ndiye mchezaji ambaye hata Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alitoa maneno ya kumtamani baada ya kufanya mambo makubwa katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Kwa mauzo ya Samatta na Berge, Genk imeingiza kiasi cha Pauni 30 milioni katika dirisha hili la Januari. Kwa Tanzania ni sawa na shilingi 89 bilioni na ushee. Imezipiga hizi pesa kimyakimya tu bila ya kelele. Kwa Genk imekuwa sehemu ya maisha ya yao kupiga pesa za mauzo ya wachezaji.
Katika dirisha kubwa lililopita ilimuuza Leandro Trossard kwenda Brighton kwa dau la Pauni 15 milioni. Ni faida juu ya faida. Haya ni maisha ya kawaida kwa Genk. Hii ni njia kubwa ya kipato kando ya viingilio, wadhamini zaidi ya sita ambao inao klabuni, pamoja na mauzo ya haki za televisheni kutoka katika michuano ya ndani na ile ya Ulaya ambayo imekuwa ikishiriki.
Genk itafanya nini na pesa hizi? Kiasi kidogo cha pesa itakiingiza tena katika usajili wa baadhi ya wachezaji ambao inajua itawauza siku za usoni kwa pesa ndefu. Kama ilivyomchukua Samatta kwa pesa ndogo, akiwa hana jina Ulaya, lakini ikamtengenezea na imepata faida kubwa kwake.
Kwanza kumbuka kwamba kuuzwa kwa kina Samatta, Berge, Trossard na wengineo sio mwisho wa timu. Kabla ya Samatta na wenzake tayari wameshawauza kina Kevin de Brune, Kalidou Koulibaly, Christian Benteke, Thibaut Courtois, Leon Bailey na wengineo wengi.
Gent ni timu ya kati ambayo kazi yake kubwa ni kusaka mataji huku ikifanya biashara nyingine ikiwemo hii hapa. Unalishangaa soka la Tanzania kwanini hatuwi na timu ambazo zina mlengo huu. Timu zetu zinaangalia zaidi mataji na sio biashara nyingine katika soka.
Bahati mbaya mataji yenyewe ni ya hasara zaidi. Mataji yanazigharimu klabu pesa nyingi na hivyo kujikuta ikitembea kwa mwendo wa hasara zaidi. Pesa inazowekeza zinaishia katika kuchukua mataji na kutambiana mitaani.
Mfumo wa Genk ni mzuri. Ukisikia Genk inatengeneza viwanja vingine vya kisasa vya mazoezi basi ni kwa pesa za mauzo ya wachezaji kama hivi na vyanzo vingine.
Inanikumbusha jinsi ambavyo Arsenal ilimuuza Nicolas Anelka mwaka 1999 kwenda Real Madrid kwa dau la Pauni 22 milioni. Wakati huo zilikuwa pesa nyingi. Nusu ya pesa zilitumika katika kujenga uwanja wa kisasa wa mazoezi wa London Colney ambao umekuwa ukiutumia hadi leo. Nusu ya pesa hizo zikatumika kumnunua Thierry Henry kutoka Juventus. Baadaye Henry alikuwa na jina kubwa kuliko Anelka.
Timu zetu zinapaswa kuwa kama Genk. Kuwa na maono ya Genk. Hatuwezi kuwa kama wao lakini tunaweza kuwa kitalu cha kuuza wachezaji kwa klabu kubwa za Afrika na kwingineko. Inashangaza kuona tunanunua wachezaji bila ya kutazama uwezekano wa kuwauza tena siku za usoni (Resale value).
Tunaleta mchezaji ana umri wa miaka 32. Anaonyesha kiwango kizuri lakini ukweli ni kwamba hawezi kuwa na soko. Klabu zetu zinapswa kupambana kuwanunua wachezaji wenye umri wa miaka 22 hadi 24 kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuwauza tena katika siku za usoni.
Tusijitoe fahamu na kushangilia uhamisho wa Samatta kutoka Genk kwenda Astoin Villa. Nyuma yake kuna funzo jingine ambalo Genk inatupa. Bahati mbaya kwa akili zetu zilivyo tunajaribu kusahau na kushangilia zaidi kumuona Samatta akicheza Villa.