Genk v Liverpool: Samatta amvaa Van Dijk

Muktasari:

Samatta kukutana na miongoni mwa mabeki bora, katika mchezo uliopita, aliiongoza KRC Genk kupata suluhu wakiwa nyumbani, Ubelgiji mbele ya Konstantino Manolas na Kalidou Koulibaly wa Napoli.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta anatarajiwa kuiongoza klabu yake ya KRC Genk katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool yenye beki bora duniani kwa sasa, Virgil van Dijk.

Samatta anategemewa katika idara ya ushambuliaji ya KRC Genk, atakuwa na kibarua kizito mbele ya beki huyo ambaye amekuwa nguzo ya Liverpool kwenye safu yao ya ulinzi, akishirikiana na Joël Matip.

Awamu hii, itakuwa ya pili kwa Samatta kukutana na miongoni mwa mabeki bora, katika mchezo uliopita, aliiongoza KRC Genk kupata suluhu wakiwa nyumbani, Ubelgiji mbele ya Konstantino Manolas na Kalidou Koulibaly wa Napoli.

Licha ya ubora wa Liverpool wakiwa na Van Dijk rekodi zao zinaonyesha ni timu ambayo inafungika, katika michezo miwili ambayo wamecheza katika hatua ya makundi, wa kwanza dhidi ya Napoli, waliruhusu mabao mawili na wa pili dhidi ya Salzburg waliruhusu mabao matatu.

Hiyo inatoa picha kama Samatta akitengenezewa nafasi za kutosha kwenye mchezo huo, anaweza kuiadhibu Liverpool kutokana na kasi ya ufungaji aliyonayo, katika michezo 10 msimu huu ya mashindano mbalimbali ameifungia KRC Genk mabao matano.

Akiuzungumzia mchezo huo kwa uchache, Samatta alisema matokeo mabaya ya mchezo uliopita katika Ligi Kuu Ubelgiji, yamekuwa sehemu ya wao kufanya zaidi kwenye maandalizi yao ya mchezo wa dhidi ya Liverpool.

“Wapinzani wetu ni imara, tumejiandaa kushinda nao ili kuweka hai matumaini yetu. Nipo tayari kukabiliana na yeyote mbele yangu, siku zote nimekuwa nikiamini uwezo wangu wa kufunga siwezi kumhofia yeyote wala kuutilia shaka,” alisema Samatta.

Samatta anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa ukanda wa Afrika Mashariki kucheza na kufunga bao kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, alifanya hivyo Septemba 17 katika mchezo ambao KRC Genk, walipoteza kwa mabao 6-2.

Katika mchezo wa leo, Liverpool watamkosa, Mohamed Salah anayeuguza majeraha ya enka ambayo yalimfanya aukose mchezo uliopita dhidi ya Manchester United, Old Trafford.